Kalonzo, Wamalwa kujiunga na kesi ya kupinga mpango wa Adani kukodi JKIA
VYAMA vitatu vya kisiasa vinataka kujiunga na kesi ya kupinga mpango wa kukodisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kampuni ya Adani kutoka India.
Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ambaye pia ni wakili mkuu, alifahamisha mahakama kuwa vyama vya Wiper Democratic Movement, Jubilee na Democratic Action Party of Kenya (DAPK) vinataka kushiriki katika kesi iliyowasilishwa na mwanaharakati Tony Gachoka na Wanasheria wa Mlima Kenya kupinga mpango huo.
Mahakama iliagiza Bw Musyoka kuwasilisha ombi rasmi, kutaka kujiunga na kesi hiyo na ikapanga kesi hiyo kutajwa Oktoba 17 kwa mwelekeo zaidi.
Wakati huo huo, Bw Gachoka na Wanasheria wa Mlima Kenya waliomba muda zaidi wa kurekebisha kesi ili kujumuisha masuala zaidi yanayohusu mpango huo.
Kupitia kwa mawakili Kibe Mungai na Ndegwa Njiru, walalamishi hao walisema korti inafaa kufikiria kutuma faili hiyo kwa Jaji Mkuu Martha Koome, ili kuteua majaji watatu kusikiliza kesi yao.
Bw Gachoka na mawakili hao wanapinga mpango wa kukodisha uwanja huo wa ndege wakisema kuwa mchakato mzima ulifanywa kwa usiri kwa vile hakukuwa na ushiriki wa umma na hiyo inaweza kusababisha kashfa.
Kampuni ya Adani imetetea makubaliano hayo katika kesi tofauti ikisema kuwa inataka kuboresha JKIA kuwa uwanja wa ndege wa kiwango cha kimataifa.