Habari za Kitaifa

Kalonzo, Wamalwa wakosoa mpango wa serikali kufidia waathiriwa wa maandamano

Na  WACHIRA MWANGI August 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MUUNGANO wa upinzani umekosoa vikali hatua ya Rais William Ruto kumteua Profesa Makau Mutua kuratibu fidia ya serikali kwa waathiriwa wa maandamano ya kupinga serikali, wakisema ni dhihaka kwa haki.

Wakizungumza katika Hoteli ya Voyager, Mombasa, kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa walisema kuwa serikali ya Kenya Kwanza haiwezi kuwa mshukiwa na wakati huo huo jaji katika kushughulikia kile walichotaja kama ukiukaji mkubwa wa haki uliofanywa na polisi dhidi ya waandamanaji, wengi wao wakiwa vijana wa Kenya.

“Ni mzaha wa hali ya juu kwa serikali inayotuhumiwa kwa kuamuru mauaji na kulemaza Wakenya sasa kuamua jinsi waathiriwa watakavyolipwa fidia. Fisi hawezi kuamua kesi ya mbuzi. Mdhulumu hawezi kutoa haki,” alisema Bw Musyoka.

Viongozi hao walitaja tafiti zinazoonyesha kuwa asilimia 86 ya Wakenya wamepoteza imani na serikali miaka mitatu tu baada ya kuichagua, wakilaumu kupanda kwa gharama ya maisha, kuporomoka kwa sekta za afya na elimu, ufisadi, na hali ya hofu inayochangiwa na utekaji na mauaji ya kiholela.

“Tumeona ajali za barabarani, kutoweka kwa watu wanaokosoa serakali, na mauaji wakati wa maandamano ya Gen Z na Sabasaba. Rais hata aliwaita vijana wetu magaidi. Hili ni suala la kitaifa, si uamuzi wa Ikulu pekee,” aliongeza Musyoka.

Kwa upande wake, Bw Wamalwa alisema uteuzi wa Prof Mutua kama Mshauri Mkuu wa Rais kama hatua ya kisiasa isiyo na msingi wa kisheria.

“Ibara ya 51(e) iko wazi. Masuala ya haki za binadamu yanapaswa kushughulikiwa na taasisi huru kama Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR), si mteule wa rais. Nafasi ya Prof Mutua haina msingi wa kikatiba na inakiuka utawala wa sheria,” alisema Waziri huyo wa zamani wa Ulinzi.

Viongozi hao walitaka mahakama kusitisha uteuzi huo na mchakato mzima wa fidia uhamishiwe kwa KNCHR.Walisisitiza kuwa fidia yoyote lazima iwe kali na iambatane na haki ya kweli, si mbinu za kisiasa za kufurahisha umma.

“Hakuna kiasi cha pesa kinachoweza kurudisha maisha yaliyopotea. Wakenya wanataka uwajibikaji, si sarakasi za kisiasa. Serikali hii imeshindwa kushughulikia ukatili wa polisi, hatutakubali uendelee,” alisema Wamalwa.

Upinzani pia ulishutumu serikali kwa upendeleo katika kushughulikia mikutano ya umma, wakidai mikutano yao huvunjwa kwa vitoa machozi ilhali mikutano ya UDA na ODM hufanyika kwa amani.

Katika uwanja wa kisiasa, viongozi wa upinzani walithibitisha mshikamano wao na kusema wamekubaliana kuunga mmoja wao tiketi ya kugombea urais mwaka wa 2027.

Muungano huo pia unajumuisha viongozi kama Martha Karua, Fred Matiang’i, Rigathi Gachagua, Mithika Linturi, na Peter Munya.Viongozi hao pia walishambulia miradi ya kuwawezesha wananchi inayofanywa na serikali, wakidai kuwa ni aibu na matumizi mabaya ya mamlaka.