Habari za Kitaifa

Karua, Kalonzo wadai Ruto na Raila wanasuka njama kuweka IEBC mfuko 

Na JUSTUS OCHIENG na NDUBI MOTURI  April 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

VIONGOZI wa upinzani Jumanne, Aprili 1, 2025 walikataa mchakato unaoendelea wa kuunda upya tume ya uchaguzi, wakishutumu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa kuuvuruga.

Viongozi hao, pia, walidai kuwa kuna kampeni za mapema na zisizo halali zinazoendeshwa na chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Dkt Ruto na Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Bw Odinga.

Wakiongozwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, mkuu wa People’s Liberation Party Martha Karua, na Eugene Wamalwa wa DAP-Kenya, walidai kuwa serikali ya Kenya Kwanza inapanga kudhibiti mchakato wa kuajiri makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Walisema kuwa mchakato wa uteuzi unavurugwa ili kuhakikisha kwamba ni watu waaminifu kwa Kenya Kwanza pekee watakaoteuliwa kwa nafasi hizo muhimu, jambo ambalo litatoa mwanya wa wizi wa kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

“Tunashangazwa na jinsi utawala wa Ruto umejizatiti kudhibiti na kuelekeza mchakato wa uajiri wa makamishna wa IEBC kwa lengo la kuteka tume inayosimamia uchaguzi.

“Huu ni mpango mchafu, ambao tunaamini unalenga kuiba kura katika uchaguzi mkuu ujao ili kuendeleza utawala wa Kenya Kwanza ambao tayari umepoteza imani ya Wakenya,” alisema Bi Karua.

Akihutubia wanahabari katika Hoteli ya Serena, Bi Karua alisema kuwa hadi sasa, “mchakato wa kuorodhesha majina umeacha nje Wakenya wenye sifa bora na uzoefu, kulingana na tathmini yetu ya waombaji zaidi ya 1,400 waliotuma maombi ya nafasi hizo.”

Wakitishia kwenda mahakamani, viongozi hao walidai kuwa baadhi ya walioteuliwa wana sifa za kutiliwa shaka na wameonyesha waziwazi kuwa na upendeleo kwa vyama vya UDA na ODM.

“Kuna madai makubwa ya ukosefu wa uadilifu na mgongano wa maslahi. Baadhi ya walioteuliwa ni wanachama wa ‘miundo’ ya uongozi ya UDA na ODM, na katika miaka mitatu iliyopita, wamefaidika na uteuzi wa upendeleo wa umma kutoka kwa Bw Ruto na Bw Odinga,” mrengo wa Bw Musyoka unaojiita People’s Loyal Coalition ulisema.

Walizungumza baada ya jopo linaloongozwa na Nelson Makanda kukamilisha mchakato wa kuwahoji walioomba nafasi ya mwenyekiti, huku mchakato wa wanaomezea mate makamishna ukiendelea.

Wanaowania uenyekiti walikuwa: aliyekuwa Msajili Mkuu wa Mahakama Anne Amadi, Saul Simiyu Wasilwa, Abdulqadir Lorot Ramadhan, Joy Mdivo, Edward Katama Ngeywa, Erastus Edung Ethekon, Francis Kakai Kissinger, Jacob Ngwele Muvengei, Lilian Wanjiku Manegene, Robert Akumu Asembo, na Charles Nyachae.

Mahojiano ya wanaotaka kuwa makamishna wa IEBC yalianza wiki iliyopita na yataendelea hadi Ijumaa, Aprili 25, 2025.

Bi Karua alitoa mfano wa Bi Joy Mdivo, ambaye alisema amekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ya Ndani ya UDA.

“Iko wazi kuwa Bi Mdivo hastahili kuteuliwa kuwa kamishna wa IEBC kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 88 (2) (a)(ii) ya Katiba ya Kenya. Ikiwa Katiba yetu inasema hivyo waziwazi, kwa nini Bi Mdivo aliwekwa kwenye orodha ya waliochaguliwa na Jopo la Uteuzi la IEBC?” alihoji.

Bw Musyoka alitaja hatua hiyo kuwa ‘uvunjaji wazi wa Katiba yetu.’

“Zaidi ya hayo, huu ni usaliti mkubwa kwa vijana wa Kenya waliotoa maisha yao mnamo Juni 25, 2024, ili kuwe na tume huru na yenye uaminifu. Wakili binafsi wa Bw Ruto pia anatarajiwa kufanyiwa mahojiano kuwa kamishna,” alisema.

Aliendelea, “Je, mtu aliyefungwa na kanuni ya siri kati ya wakili na mteja wake anawezaje kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kwa njia isiyo na upendeleo ikiwa atateuliwa?”

Bw Wamalwa alisema kuwa inazidi kudhihirika kuwa orodha ya awali ilifanyiwa marekebisho ili kuingiza watu wenye uhusiano wa kisiasa na serikali.

“Mbaya zaidi, kuna wasiwasi unaozidi kuongezeka kuhusu Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), ambayo hivi karibuni imeshutumiwa kwa utekaji nyara, mateso, watu kutoweka, na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu.

“Tunatoa changamoto kwa Jopo la Uteuzi la IEBC kueleza kwa uwazi jinsi Bi Mdivo na Katwa Kigen walivyoorodheshwa, na pia kufafanua jukumu la NIS katika mchakato huu.”

Viongozi hao wa upinzani pia waliitaka jopo hilo kutojihusisha na vitendo vyovyote vya upendeleo ambavyo vinaweza kuhatarisha haki za uchaguzi nchini Kenya.

“Jopo linapaswa kuteua tu watu ambao hawana doa na ambao watafanya kazi zao kwa mujibu wa Katiba ya Kenya.”

Viongozi hao pia walisisitiza kuwa kanuni ya mashauriano na makubaliano itekelezwe kabla ya uteuzi wa mwisho wa makamishna kati ya Bw Ruto, Bw Odinga, na upinzani ili kuakisi hali halisi ya kisiasa nchini.