Kenya na Burundi kupata chanjo ya Mpox kutoka Ujerumani, Nigeria ikipokea dozi 10,000
Lagos, Nigeria
NIGERIA imepokea shehena ya kwanza ya dozi 10,000 za chanjo dhidi ya homa ya nyani (Mpox) iliyotolewa kama msaada na Amerika katika juhudi kuzuia msambao wa ugonjwa huo.
Taifa hilo la Afrika Magharibi tayari limeripoti zaidi ya vifo 40 na visa 830 vya maambukizi ya ugonjwa huo katika majimbo 13.
Chanjo hiyo imetolewa baada Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kutangaza Mpox kama tishio kubwa la kiafya ulimwenguni
Balozi wa Amerika Richard Mills alisema kuwa Nigeria imejiandaa vizuri kutumia chanjo hizo.
“Nigeria imeweka mipango ya utoaji chanjo,” akasema.
“Kuna mipango ya namna ya kutumia chanjo hizi vizuri, namna ya kuhakikisha kuwa tunafaidi kutokana na dozi hizi 10,000. Ndio sababu Nigeria imeteuliwa kupokea shehena ya kwanza ya chanjo hiyo,” Mills akaeleza.
Mnamo Jumatano, Agosti 28, 2024, Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Afrika kilisema zaidi ya vifo 620 vimeripotiwa kutokana na Mpox katika nchi 13 za wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
Mkurugenzi wa Afrika ya Msingi, Muyi Aina anasema idara yake itayapa kipaumbele majimbo yenye visa vingi vya Mpox katika mchakato wa usambazaji wa chanjo hiyo.
“Mengi ya majimbo hayo yenye idadi kubwa ya visa vya maambikizi yako Kusini mwa Nigeria. Tutashirikiana na majimbo hayo kutengeneza mipango mahsusi kuhakikisha kuwa chanjo zinafikia watu wote walioko katika hatari ya kuambukizwa.
Mwakilishi wa WHO nchini Nigeria, Walter Mulombo alisema kuwa shughuli ya utoaji chanjo itaanza hivi karibuni “licha ya kwamba baada ya watu huhofia kujitokeza kwa shughuli kama hiyo.”
Huku ugonjwa wa Mpox ukienea katika mataifa ya Afrika ya Kati na Afrika Magharibi, mataifa ya kigeni yanaendelea kujitokeza kutoa msaada wa chanjo na mahitaji.
Kwa mfano, Ujerumani inapanga kutoa msaada wa dozi 100,000 za chanjo kwa mataifa ya Afrika Mashariki.
Nchi za Burundi na Kenya zimeripoti visa vya Mpox katika siku za hivi karibuni.