Habari za Kitaifa

Knut yaitaka TSC iajiri washauri kuzuia visa vya walimu kujitia kitanzi

Na VITALIS KIMUTAI December 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha walimu (KNUT) kinataka Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) iajiri washauri nasaha kushughulikia visa vya kujitia kitanzi na matumizi mabaya dawa za kulevya kwa walimu.

TSC inasema walimu wengi wanahangaishwa na magonjwa ya akili, hali ambayo imeathiri utendakazi wao na kusambaratisha familia zao.

Mwakilishi wa Kike wa Kwanza wa Kitaifa Mercy Ndung’u amesema maelfu ya walimu wanaumia lakini wao huwa wananyamaza tu.

“Walimu wanahitaji huduma za ushauri popote walimu nchini. Ni huduma ya lazima ambayo inafaa kutolewa na wizara na mwaajiri ili kuokoa maisha,” Bi Ndung’u akasema katika hafla ya kuadhimisha siku 16 ya kukabili dhuluma za kijinsia mjini Bomet mwisho wa juma.

“Baadhi ya changamoto za walimu huwasababisha kujihusisha na utumizi mbaya wa dawa za kulevya ili waepuke hali halisi ya maisha. Ni suala ambalo linafaa kuangaziwa na washikadau wote wa elimu nchini,” akaongeza.

Kauli yake ilikaririwa na mwanachama wa Baraza Kuu la Utendaji (NEC) Alice Bor, Katibu Mtendaji wa KNUT tawi la Bomet Desmond Langat, naibu wake Jeff Bett na mwakilishi mwanamke wa KNUT tawi la Bomet Betty Langat.

“Baadhi ya walimu wamejiua sababu ya msongo wa mawazo, wengine wametelekeza wajibu huku baadhi wakianza uraibu wa pombe baada ya kukosa msaada wa kisaikolojia,” akasisitiza Bw Langat.

Naye Bw Bett akasema: “Walimu wanahitaji msaada kutoka kwa washikadau wote katika jamii. Hatufai kupuuza changamoto ambazo zinawakabili walimu nchini.”

Walisema walimu wamekuwa wakipelekwa katika vituo vya kurekekebisha tabia nchini na wakarejea wakiwa wameimarika huku wengine wakiishia kusumbuka tena.

Bi Langat alidokeza kuwa walimu wengine wanaishi bila waume ama wake sababu ya kifo ama utengano; suala ambalo anasema halifai kupuuzwa.

TSC imekuwa ikikabili suala la ulevi na mafadhaiko miongoni mwa walimu kwa miaka kwa kuwa limeathiri utendakazi katika shule za umma.

Tukio la hivi karibuni zaidi cha kujitia kitanzi cha mwalimu wa shule ya upili ya Kenya High jijini Nairobi.

Mwili wake ulipatikana ukining’inia katika ngazi ya tenki ya maji shuleni humo mnamo Oktoba 2, 2024.

Mwalimu mwingine wa shule ya upili huko Nyamira alijitia kitanzi Juni 6, 2024 baada ya kupoteza pesa katika mchezo wa kamari.

Kabla ya hapo, mwalimu wa shule ya upili ya Senior Chief Musa Nyandusi – Kegati, Evans Onchari alijiua mnamo Februari 13, 2023.

Katika barua aliyoacha, alisema hali mbaya ya afya ilimsukuma kusitisha maisha yake.

IMETAFSIRIWA NA LABAAN SHABAAN