Habari za Kitaifa

Kundi la wanawake lilivyotua jijini kwa magunia ya nailoni kuandamana dhidi ya utekaji nyara   

Na SAMMY WAWERU January 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUNDI moja la wanawake Jumatatu, Januari 6, 2025 lilitua Jijini Nairobi likiwa limevalia magunia ili kushiriki maandamano dhidi ya utekaji nyara.

Kina mama hao waliokongamana Kimathi Street, walikuwa wamevalia magunia ya nailoni.

Walilenga kuungana na vijana na wanaharakati waliotishia kushiriki maandamano Jumatatu, wakishinikiza kuachiliwa kwa watu waliotekwa nyara.

“Mama ndiye anaelewa uchungu wa kuzaa na kulea mtoto, na ndio maana tumejumuika hapa kuhimiza serikali iachilie watoto wetu,” alisema mmoja wa kina mama hao.

Kundi la kina mama waliovalia magunia waliokongamana Kimathi Street, Nairobi kushiriki maandamano ya kutaka kuachiliwa kwa vijana waliotekwa nyara. PICHA|SAMMY WAWERU

Maafisa wa usalama waliotumwa kushika doria, hata hivyo, waliwaonya dhidi ya kufanya maandamano.

Likijitetea, kundi hilo lilihoji shabaha yao ni kushiriki maandamano yatakayosheheni maombi.

Aidha, walikuwa wamebeba Biblia na hawakuruhusu jinsia ya kiume kujiunga nao.

“Hatutaki wanaume kujumuika nasi,” walisisitiza.

“Ikiwa ni maombi, ni sawa. Maandamano ndiyo hayataruhusiwa. Kwa nini jana (Jumapili) hamkufanya maombi kama Wakenya wengine?” afisa wa polisi aliyesimamia kikosi cha waliotumwa barabara ya Kimathi alitaka kujua.

Afisa wa polisi akizungumza na mmoja wa wanawake waliovalia magunia na kufika Jijini Nairobi, kwa lengo la kushiriki maandamano kushinikiza kuachiliwa huru kwa vijana waliotekwa nyara mwishoni mwa 2024. PICHA|SAMMY WAWERU

Wakitoa sala, waliskika wakiombea waliotekeleza utekaji nyara kuwa na utu.

“Mwenyezi Mungu tunakusihi ulinde watoto wetu…Na kwenu watoto, tunawashauri muwe na heshima kwa wakubwa wenu na viongozi,” waliomba.

Wanawake hao walijumuisha wa dini ya Kikristu na Kiislamu.

Kabla ya kushiriki maombi, waliopakata Biblia waliziinua juu ishara ya kumlilia Mungu vijana waliotekwa nyara waachiliwe huru na wakiwa salama.

Magunia waliyovalia, walisema yaliashiria kumbukumbu za taifa enzi za ukoloni kukomboa Kenya kutoka mikononi mwa Mbeberu.

Mojawapo ya Biblia walizokuwa nazo kina mama hao waliovalia magunia ya nailoni. PICHA|SAMMY WAWERU

“Yana maana kuwa tumejitokeza kwa njia ya maombi kulilia Mungu aokoe vijana wetu,” mmoja wa kina mama hao akaambia Taifa Dijitali tulipodadisi kujua.

Jumatatu asubuhi, Januari 6, baadhi ya vijana waliotekwa nyara waliachiliwa huru bila kushtakiwa kwa uhalifu wowote.

Hata hivyo, haijajulikana ni kina nani waliowateka Huduma ya Polisi ya Kitaifa (NPS) kupitia Inpekta Jenerali Mkuu wake, IG, Douglas Kanja maafisa kutohusika na visa hivyo.

Licha ya Rais William Ruto kuahidi kwamba serikali yake haitajipaka tope kwa kutekeleza utekaji nyara kwa Wakenya wanaokosoa utawala wake, Jumapili, Januari 5, 2025 katika ibada ya Kanisa Kaunti ya Baringo, baadhi ya viongozi wa kisiasa wandani wake waliskika kutojali kuhusu visa vinavyoshuhudiwa.

Wanawake hao waliovalia magunia ya nailoni wakishiriki maombi. PICHA|SAMMY WAWERU

Vijana waliotoweka, inasemekana ni miongoni mwa wanaokosea viongozi serikalini kwa kuchapisha vibonzo vinavyowakosea heshima.

Mbunge wa Kapseret, Bw Oscar Sudi akizungumza Baringo, alisema kwamba endapo Wizara ya Usalama wa Ndani ingekuwa chini yake ingemchukua siku tatu pekee kutia adabu vijana waliokosa nidhamu kwa viongozi.

Matamshi ya mwanasiasa huyo ambaye ni mwandani wa Rais Ruto, hata hivyo, hayajapokelewa vyema na wanaokosoa serikali ya sasa wakidai “yanaashiria serikali ndiyo inaendesha utekaji nyara.”