Habari za Kitaifa

Mabalozi wa EU wamtaka Ruto akomeshe utekaji nyara wa wakosoaji

Na STEVE OTIENO November 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MABALOZI kutoka mataifa ya Muungano wa Ulaya (EU) wamemtaka Rais William Ruto ahakikishe kuwa utawala wake unaheshimu sheria na kukomesha visa vya utekaji nyara, raia kukamatwa kiholela na wengine kupotea kwa njia ya kutatanisha, ambavyo vimeongezeka nchini.

Kupitia taarifa, mabalozi hao wamesisitiza lazima kuwapo uchunguzi ili waliohusika na kamatakamata kinyume cha sheria na utekaji nyara wakabiliwe kisheria.

Taarifa hiyo ilitiwa saini na mabalozi kutoka Denmark, Finland, Ujerumani, Ireland, Uholanzi, Norway, Uswidi, Uswizi na Uingereza.

Mabalozi hao walisema katiba imeweka wazi mkondo wa sheria ambao unastahili kufuatwa iwapo raia amekosa wala hakuna kifungu kinachosema auawe bila kupewa nafasi ya kujitetea.

“Katiba inasisitiza kuhusu haki za kila raia kwa hivyo matukio mengi ya watu kupotea katika njia tatanishi na wengine kukamatwa licha ya uamuzi wa korti, hayafai,” wakasema mabalozi hao.

Waliongeza kuwa Rais Ruto amenukuliwa hadharani akisema hapo awali kuwa visa hivyo havingetokea kwenye utawala wake hivyo basi ni wakati mwafaka kwake kuhakikisha ahadi hiyo inatimizwa.

Taarifa hiyo ilitolewa baada ya Balozi wa Amerika Meg Whiteman kughadhabishwa na ufichuzi kuwa kampuni za mawasiliano sasa zinatoa maelezo ya Wakenya ambayo yanatumika kusaidia kufanikisha utekaji nyara na mauaji yanayotekelezwa na vyombo vya usalama.

“Sheria kuhusu siri za maelezo yanayomhusu mtu na haki za raia lazima iheshimiwe,” akasema Whitman wakati wa mahojiano na wanahabari mjini Kitale ambako alikuwa akikutana na mashirika ya haki ya eneo hilo.

Bi Whitman alisema Amerika iko tayari kushirikiana na mashirika ya umma kuhakikisha haki ya raia inaheshimiwa na akautaka utawala wa Kenya Kwanza uhakikishe kuwa unachukua hatua dhidi ya wanaokiuka haki za kibinadamu.

Taarifa ya mabalozi hao imetolewa wakati ambapo Kenya imekuwa ikishuhudiwa kupanda kwa visa vya raia kuuawa, kutekwa nyara na kukamatwa kiholela. Wale ambao wamekuwa wakilengwa sana ni wakosoaji wa serikali na watetezi wa haki za binadamu.

Kisa cha hivi punde ni kukamatwa kwa mwanaharakati Boniface Mwangi nyumbani kwake Machakos kisha kuzuiliwa kwake katika Kituo cha Polisi cha Kamukunji.

Bw Mwangi ambaye aliitisha maandamano jijini Nairobi mnamo Oktoba 26, aliachiliwa baada ya kusota seli bila kushtakiwa kortini.

Diwani kutoka Wajir Yusuf Hussein Ahmed ambaye alitekwa nyara Nairobi siku 49 zilizopita bado hajapatikana, polisi nao wakisema hawajui aliko.

Mnamo Septemba mashirika ya kupigania haki za kibanadamu yalitoa ripoti jinsi mauaji yalivyotokea wakati wa maandamano ya Gen-Z mnamo Juni 25 siku ambayo walivamia majengo ya Bunge.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu sita waliuawa huku wengine 72 wakitekwa nyara au kutokomea kwa njia za kutatanisha. Wakati wote wa maandamano hayo yaliyochukua miezi miwili, kulikuwa na mauaji ya watu 61 katika maeneo mbalimbali nchini.

Mapema wiki hii, Mkurugenzi wa Shirika la Kijasusi Amerika, William Burns alikutana na Rais Ruto ambapo alisema taifa lake liko tayari kusaidia Kenya kuimarisha idara zake za ujasusi.

Burns ambaye alikuwa akizuru Kenya mara ya pili baada ya kufika nchini mnamo Januari, alimtaka Rais Ruto ahakikishe kuwa visa vya watu kupotea kwa njia tata na wengine kuuawa kiholela, vinakomeshwa.