Magharibi wataka Oparanya achukue kiti cha Kindiki 2027
WABUNGE kutoka Magharibi mwa nchi sasa wanataka Profesa Kithure Kindiki aondolewe kama mgombeaji mwenza wa Rais William Ruto mnamo 2027 na nafasi hiyo ikabidhiwe Wycliffe Oparanya.
Wakiongea katika eneobunge la Khwisero, viongozi hao walisema kuwa waziri huyo wa vyama vya ushirika na biashara ndogo ndogo ndiye anatosha kuwa mgombea mwenza wa rais mnam0 2027.
Wabunge Christopher Aseka (Khwisero), Titus Khamala (Lurambi), Bernard Shinali (Ikolomani), Emmanuel Wangwe (Navakholo) na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kakamega Elsie Muhanda, walisema Bw Oparanya ana uzoefu unaoweza kumsaidia Rais Ruto kurejesha nchi kwenye mkondo wa kuridhisha.
Viongozi hao walitaja rekodi ya Bw Oparanya akiwa gavana wa Kakamega kati ya 2013-2022 na alipokuwa waziri wa mipango ambapo aliweka msingi wa Ruwaza ya 2030 kama sifa faafu.
Huku wakisisitiza kuwa mara hii hawatalegeza kamba, viongozi hao waliahidi kuwa jamii ya Mulembe itampa Rais kura 2027 iwapo Oparanya atakuwa mgombeaji mwenza.
Aidha, wanasiasa hao walisema kuwa eneo la Mlima Kenya limeonyesha maasi ya wazi dhidi ya Rais Ruto na halifai kutengewa wadhifa wa mgombeaji mwenza. Hii ni baada ya kuondolewa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwenye wadhifa wake Oktoba mwaka jana.
Kauli ya wabunge hao inajiri wakati ambapo rais anatarajiwa kutembelea Mlima Kenya wiki mbili zijazo. Pia, Rais Ruto amekashifiwa kuwa na mkono fiche katika kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza.
“Kwa sababu tunamuunga mkono Rais Ruto amalize muhula wake wa miaka 10, sisi tunaidhinisha Bw Oparanya awe mgombea mwenza wake 2027,” akasema Bw Aseka.
Mbali na mipango ya ugombeaji wenza, Bw Aseka alisema mipango inaendelea ya kumkweza Bw Oparanya na kumtawaza kama kigogo wa siasa za eneo hilo.
Mbunge huyo alisema eneo la Magharibi limekuwa pembeni katika siasa za Kenya na viongozi wao wamekuwa wakiingia serikalini kupitia mlango wa nyuma.
“Bw Oparanya ni waziri kwa kuwa alipata wadhifa huo kupitia dirishani. Namwomba gavana huyo wa zamani awe mstari wa mbele ili awe naibu rais mnamo 2027,” akaongeza Bw Aseka.
Bi Muhanda naye alisema eneo la Magharibi lina idadi ya juu ya wapigakura na linastahili kuwa mstari wa mbele wakati wa kuamuliwa kwa masuala ya kitaifa.
“Tumekutana na ndugu na dada zetu kutoka Bungoma, Busia na Vihiga na wote wamekubali kumuunga Bw Oparanya. Tutawasilisha pendekezo hili kwa rais ili aanze kuifanyia kazi mapema,” akasema Bi Muhanda.
“Huu ndio wakati wa Magharibi kuungana na kusaka nafasi yetu kitaifa. Oparanya anatosha kuwa naibu rais na tunamhakikishia uungwaji mkono,” akasema Bw Wangwe.
Bw Khamala naye alisema kuwa jamii hiyo haiwezi kuendelea kukosa mwelekeo na dira na la muhimu ni wasimame wima nyuma ya Bw Oparanya.
Kauli ya wanasiasa hao inatarajiwa kumweka pabaya Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangúla ambao wanaonekana kama viongozi ambao wana usemi mkuu kwenye utawala wa Kenya Kwanza.
Imetafsiriwa na Cecil Odongo