Makundi nusura yapigane Eldoret yakibishania Murkomen, Kindiki na Duale kurudishwa kazini
POLISI mjini Eldoret mnamo Jumatano waliwatawanya mamia ya vijana waliokuwa wakiandamana kwenye barabara ya Eldoret-Kapsabet wakitaka Rais William Ruto awarejeshe kazini aliyekuwa Waziri wa Barabara na Uchukuzi Kipchumba Murkomen pamoja na waliokuwa Mawaziri wa Mambo ya Ndani na Ulinzi, Kithure Kindiki na Aden Duale mtawalia.
Vijana hao ambao walikuwa wakiimba nyimbo za kusifu Murkomen, Kindiki na Duale walidai kuwa watatu hao walikuwa miongoni mwa mawaziri waliofanya kazi vyema kabla ya kufutwa na rais Ruto.
“Kindiki, Murkomen na Duale walionyesha umahiri katika kipindi walichohudumu katika baraza la mawaziri na Rais Ruto anapaswa kuwarejesha kazini atakapoteua baraza lake la mawaziri,” mmoja wa waandamanaji alisema.
Huku wakiwa wamebeba mabango ya kuwasifu watatu hao, vijana hao walidai kuwa hatua ya kuvunja baraza zima la mawaziri ilichochewa kisiasa na wanasiasa waliojificha nyuma ya vijana wa Gen Z.
“Tunataka Murkomen, Kindiki na Duale warudi. Wao ni safi na rekodi yao inajieleza yenyewe,” alisema Charles Kimeto, mmoja wa waandamanaji.
Polisi waliwazuia waandamanji hao kuingia katikati mwa mji wakihofia kutokea makabiliano kati ya kundi jingine lililokuwa likiunga mkono kuondolewa kwa mawaziri hao watatu.
“Hatuwezi kuwaruhusu kuingia katikati mwa jiji, wanaenda kugongana na kundi pinzani ambalo linawasubiri karibu na hoteli ya Members,” mmoja wa mafisa wa polisi waliotibua maandamano hayo,” alisema.
Waandamanaji hao waliojumuisha waendesha bodaboda walitorekea usalama wao kuelekea eneo la Elgon View kupitia barabara ya Nairobi pale polisi walipowakabili.
Kundi pinzani lilidai kuwa waandamanaji hao walikuwa wamelipwa na wanasiasa fulani kutoka eneo hilo ili kuunga mkono mawaziri husika.
“Hawa ni waandamanaji walionunuliwa, kwa vile sisi kama Gen Z tumempa rais Ruto mpango wa kuashiria nani anafaa kuteuliwa kuwa waziri. Kelele hizi hazitabadilisha chochote,” alisema mmoja wa waandamanaji wa Gen Z ambaye alikuwa miongoni mwa timu iliyokuwa ikingojea kundi pinzani.