Habari za Kitaifa

Maswali kampeni za Raila kwa kiti cha AUC zikikaukiwa na pesa

Na JUSTUS OCHIENG November 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

KAMPENI za Kinara wa Upinzani Raila Odinga za uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) zimekumbwa na mawimbi makali baada ya ufichuzi kuibuka kuwa kamati husika haijapewa pesa za kutosha na serikali.

Maswali yameibuka kuhusu iwapo serikali kwa kweli imetenga bajeti kwa shughuli hiyo na iwapo ina nia nzuri kuhakikisha anafanikiwa au la.

Siku nne tu baada ya Bw Odinga kuzindua kampeni yake ambapo aliweka wazi maono yake kuhusu Afrika, Taifa Leo imebaini kuwa kuna ‘njaa’ kubwa na ‘ukame’ wa pesa katika sekretariati inayoongoza kampeni hizo.

Ukosefu wa fedha huenda ukakatatiza kampeni za Raila za kuzunguka Afrika na kuyashawishi mataifa mbalimbali yampigie kura. Hii ni kwa sababu kampeni hizo huwa ni kali na huhitaji pesa nyingi na rasilimali tele ili kuzifaulisha.

Kati ya gharama hizi ni za usafiri, kuandaa mikutano na ili kufanya mazungumzo na mabalozi na marais wa Afrika, ukosefu huo wa fedha umeingiza kiwewe sekretariati ambapo wanachama wake hawajapokea malipo yao ya kila mwezi hadi leo.

Wakati ambapo kampeni za Raila ilizinduliwa mnamo Agosti 27 kwenye ikulu ya Nairobi, Rais William Ruto pia alizindua sekretariati inayoongozwa na Katibu katika Wizara ya Masuala ya Kigeni Dkt Korir Sing’oei na aliyekuwa Balozi wa Kenya Amerika Elkanah Odembo.

Kwenye mahojiano ya awali, Dkt Sing’oei alisema serikali itatenga bajeti ya kugharimia kampeni hizo.

Hapo jana, mahojiano na wanachama wa sekretariati ya Bw Odinga yalisawiri uchechefu wa hela na inapotolewa huwa ni kugharimia tu kampeni za Raila mwenyewe huku wao wakiacha bila chochote.

Kuna madai kuwa baadhi ya asasi za serikali ambazo hazijulikani zimekuwa zikipokea pesa na kugharimia safari za Raila pekee huku sekretariati yake ikitegemea hisani za wasamaria wema.

Duru zinaarifu kuwa asasi ya kiusalama ya serikali sasa imetwaa majukumu ya sekretariati na sasa ndiyo inaendesha kampeni hizo.

“Ni jambo linalosikitisha sana. Mambo si mazuri jinsi ambavyo watu wanafikiria na hofu yetu ni kuwa huenda ikasemekana kitita kikubwa kilitumika baada ya kampeni kukamilika na hatutakuwa na njia ya kujitetea.”

Baadhi ya wafanyakazi katika sekretariati hiyo inadaiwa waliachwa nje ya uzinduzi kule Addis Ababa wiki jana kutokana na kucheleweshwa kwa mipango ya kuhakikisha wanasafiri hadi Ethiopia.

Taifa Leo ilifahamishwa kuwa mchakato wa kuhakikisha kuwa Bw Odinga anapewa ndege ya kibinafsi ya kuzuru Afrika pia haujakamilishwa hadi leo akilazimika kutumia ndege za uchukuzi wa kawaida.

Hii ni licha ya kuwa imesalia miezi miwili pekee kabla ya kura hiyo kufanyika mnamo Februari kupata mrithi wa Mousa Faki Mahamat.

Wapangaji mikakati ya Bw Odinga wanaamini kuwa ndege hiyo itamsaidia Bw Odinga kuzunguka Afrika bila tatizo lolote na kuwafikia marais wote.

“Gharama kubwa ni kukodisha ndege ya kibinafsi ambayo ni Sh77 milioni na tumepokea maombi kutoka kwa kampuni kadhaa ambazo ziko tayari kutoa ndege za kukodisha.”

Taifa Leo pia ilibaini kuwa mgao wa bajeti ya kufadhili kampeni hizo ulipitishwa na Baraza la Mawaziri lakini jinsi pesa hizo zinavyotumika ni fumbo kwa sababu hawazioni.

“Ninafahamu baraza la mawaziri lilitenga pesa za kampeni ila ukitaka kuthibitisha ni serikali yenyewe itafanya hivyo. Katika sekretariati bado tunasuburi kupokea malipo yetu ya kila mwezi, tuko njaa.”

Juhudi zetu za kufikia Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni na Bw Sing’oei ili wazungumze kuhusu ukame wa pesa katika kampeni za Raila hazikufaulu.

Bw Mudavadi ambaye yuko jijini Baku, Azerbaijan kwa Kongamano la COP29 kumwakilisha Rais Ruto hakujibu ujumbe wa Taifa Leo.

Hali ilikuwa hiyo hiyo kwa Dkt Sing’oei na Bw Odembo pia hakutoa mwanga kuhusu suala hilo.

Bw Odembo alisema kuwa wiki ijayo Bw Odinga atakuwa na mkutano na viongozi wapangaji mikakati Afrika ili kutoa ufafanuzi kuhusu ajenda zake na kushirikiana nao kuhakikisha anafaulu kwenye azma yake.

Akiongea jijini Addis Ababa, Ethiopia wikendi, Bw Raila aliamua kuvumisha Azimio la AU la 2063 ambalo madhumuni yake makuu ni kuhakikisha Afrika inakuwa taifa moja litakalokuwa na jukwaa bora la kusukuma ajenda yake kwenye maelewano na nchi nyinginezo duniani.