Mlima mbioni kusaka mrithi wa Gachagua asiposhinda kesi ya kung’atuliwa
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua anakabiliwa na hatari ya kuzuiwa kushiriki katika chaguzi kuu mbili zijazo endapo mahakama haitabatilisha kutimuliwa kwake.
Hii ni kwa mujibu wa kipengele cha 75 cha Katiba ya sasa ambacho kinasema kiongozi ambaye ameondolewa afisini kwa kosa la ukiukaji wa Katiba na sheria za nchi haruhusiwi kushikilia wadhifa wa umma kupitia uchaguzi au uteuzi kwa angalau miaka 10.
Hali hiyo ikitokea, kuna uwezekano mkubwa kuwa eneo la Mlima Kenya litabaki mayatima kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Katika hali kama hii, eneo hilo litalazimika kuanza kumtafuta mrithi wa Bw Gachagua ambaye, kabla na hata baada ya kuondolewa afisini, bado yeye ndiye mwanasiasa mwenye ushawishi mwingi miongoni mwa raia.
Itakumbukwa kuwa mnamo 2013, nusra eneo la Mlima Kenya lijipate katika hali kama hiyo ilipodaiwa kuwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta asingeruhusiwa kuwania urais kwa misingi ya tuhuma zilizompata katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC).
Dhana hiyo ilisababisha woga miongoni mwa maafisa fulani serikalini kiasi cha wao kuibua mipango ya kuanza kumwandaa Musalia Mudavadi kuwa mrithi wa Rais Mwai Kibaki.
Wazo hilo lilitupiliwa mbali baada ya mawakili fulani wepevu kushauri kwamba Bw Kenyatta, ambaye alishtakiwa pamoja na Rais William Ruto na Wakenya wengine wanne, asingezuiliwa kuwania urais kwa sababu hakuwa amepatikana na hatia.
Sasa mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru anaelezea hofu kuwa Bw Gachagua atazimwa kuwania urais 2027 na hivyo wakazi wa Mlima Kenya watakosa kiongozi watakayempigia kura.
Msimamo mkali wa Bw Gachagua
“Binafsi nilimshauri Gachagua asisubiri aondolewe afisini bali ajiuzulu mapema ili awe na nafasi ya kuwania katika uchaguzi mkuu wa 2027. Lakini alikataa.
Aliniambia kuwa yeye si mtu mwenye ubinafsi ambaye haja yake kuu ni kuwania urais 2027 pekee,” akasema mbunge huyo ambaye ni mmoja wa wandani wa karibu wa Bw Gachagua.
Akaongeza: “Bw Gachagua aliweka wazi kuwa haikuwa lazima kwake kuwania, kwamba anaweza pia kumuunga mkono mtu mwingine.”
Ilivyokuwa nyakati za masaibu ya ICC yaliyomzonga Bw Kenyatta mnamo 2013, kuna baadhi ya watu ambao wanafurahia masaibu ya Bw Gachagua.
Seneta wa Murang’a Joe Nyutu anawataja viongozi hao kuwa wasaliti “wasio na aibu wanaposakata densi kwenye ‘kaburi’ la mwana wao.”
“Tunashangaa kuwa watoto wetu wamejitokeza kuwa wasaliti wa Gachagua huku wakisherehekea masaibuyake kwa matarajio kuwa Ikulu itawasaidia kutwaa nafasi ya Gachagua ambaye ndiye msemaji wa Mlima Kenya,” akaeleza Seneta Nyutu akiongeza kuwa wanasiasa hao wako katika Bunge la Kitaifa na Seneti.
Mnamo 2013 wakati wa masaibu yaliyomfika Kenyatta, wanasiasa kama vile Jeremiah Kioni (sasa Katibu Mkuu wa Jubilee), Peter Kenneth, Martha Karua (kiongozi wa sasa wa Narc Kenya), Paul Muite na Bi Winnie Kaburu walisawiriwa kuwa viongozi mbadala.
Lakini kuhusiana na masaibu yanayomzonga Gachagua wakati huu, hakujatokea mmoja wa wandani wake ambaye anaweza kuchukua nafasi yake endapo atazuiwa kuwania urais 2027.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga