Habari za Kitaifa

Mlima wa madeni Kenya ikiendea mkopo wa Sh195 bilioni Uarabuni

Na REUTERS September 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Kenya inatarajiwa kutia saini makubaliano ya kuiwezesha kupata mkopo wa kima cha dola 1.5 bilioni (Sh195 bilioni) kutoka kwa Milki ya Umoja wa Kiarabu (UAE) za kusaidia kufadhili shughuli za maendeleo.

Duru zimeiambia shirika la habari la Reuters kwamba mkopo huo utatozwa riba ya kima cha asimilia 8.2.

“Kenya inapanua mawanda yake katika juhudi zake za kusaka fedha za kuziba pengo katika bajeti yake,” afisa mmoja wa Wizara ya Fedha akasema, akiongeza kuwa “makubaliano hayo yamekamilishwa.”

Hata hivyo, Wizara ya Fedha ya UAE na Benki Kuu ya nchi hiyo hazikusema chochote kuhusu suala hilo zilipoombwa kutoa kauli.

Waziri wa Fedha wa Kenya John Mbadi na maafisa wengine wa ngazi za juu katika wizara hiyo hawakupatikana kutoa kauli.

Serikali ya Kenya imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kupata fedha za kufadhili shughuli zake tangu Julai 1, mwaka huu baada maandamano ya vijana wa Gen Z kulazimisha Rais William Ruto kuondoa Mswada wa Fedha wa 2024 uliotarajiwa kuisaidia kukusanya mapato ya kima cha Sh346 bilioni.

Kucheleweshwa kwa ufadhili kutoka kwa Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) kumeiongezea Kenya changamoto za kifedha.

Inakadiriwa kuwa Kenya sasa inatarajiwa kuwa na pengo la Sh989 bilioni katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2024/2025 ikilinganishwa na Sh642 bilioni kabla ya maandamano ya Juni mwaka huu.

Mnamo Jumatano wiki hii shirika la habari la Bloomberg liliripoti kuwa Kenya ilikuwa inafanya mazungumzo na UAE kuhusu mkopo huo.

Chini ya utawala wa Rais William Ruto ambao ulianza Septemba 13, 2022, Kenya imejenga uhusiano mzuri na Milki hiyo ya UAE.

Kampuni za mafuta za Abu Dhabi National Oil Company (ADNOC) na Emirates National Oil ni miongoni mwa kampuni tatu za eneo la Ghuba zilizoteuliwa na utawala wa Ruto mwaka jana kuiuzia Kenya kwa masharti nafuu.

Chini ya mpango huo serikali inapewa muda mrefu kulipia mafuta hayo tofauti na mpango wa zamani ambapo ilitarajiwa kulipa muda mfupi baada ya kuuziwa bidhaa hizo.

Mnamo 2018 UAE iliipa Ethiopia mkopo wa dola bilioni moja (Sh129 bilioni) kuisaidia kukabiliana na changamoto za kifedha.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga