Habari za Kitaifa

Msipotulipa deni la NHIF, itakuwa vigumu kutumia hospitali zetu mkianzisha SHIF – Magavana

Na KENNEDY KIMANTHI, ERIC MATARA August 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAGAVANA wanaitaka Wizara ya Afya kupatia kipaumbele malipo ya Sh8 bilioni ambazo Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Kitaifa (NHIF) inadaiwa na hospitali za kaunti kabla ya kuhamia katika Hazina ya Afya ya Jamii (SHIF).

Wamesisitiza kuwa kukamilisha kulipa malimbikizi hayo ni muhimu ili kuepuka misukosuko ya kifedha katika vituo vya afya vya umma ambavyo tayari vimelemewa na mzigo wa deni.

Miezi kadhaa baada ya hospitali za kibinafsi kote nchini kuondoa huduma zao kwa Wakenya walio na kadi za NHIF kutokana na deni lingine, ni hospitali za umma za kaunti pekee zinazokubali kadi za NHIF na kuwalazimu Wakenya kutoka jamii maskini kufurika katika hospitali za umma kusaka huduma za afya.

Magavana wameonya kuchelewesha kumaliza kulipa deni hilo kutawasababishia mateso zaidi Wakenya wenye mapato ya chini wanaotegemea huduma hizo.

Kaunti za Nairobi na Nakuru ni miongoni mwa zinazodai NHIF kiasi kikubwa cha pesa huku Nairobi ikidai kiasi kisichopungua Sh2.1 bilioni na Nakuru Sh540 milioni kutoka kwa NHIF na Linda Mama.

“Tunapohamia SHIF, hatutaki kuona hali ambapo Sh8 bilioni zinageuka kuwa malimbikizi ya deni ambalo halijalipwa kwa vituo vya afya. Tunataka NHIF ilipe vituo ambavyo madeni yake yangali hayajalipwa. Ni kwa namna hiyo tu tutaweza kuhamia SHIF bila deni lolote linalodaiwa na vituo vya kaunti,” Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika Baraza la Magavana, Gavana Muthomi Njuki alisema Jumanne.

Gavana wa Nakuru, Bi Susan Kihika, alielezea wasiwasi wake, akisema Nakuru pekee inadai NHIF na mpango wa Linda Mama kitita cha Sh540 milioni.

“Hali ya kukosa kulipa ni mzigo mzito mno kwa hospitali zetu na huenda hivi karibuni ikalemaza oparesheni. Tunahimiza Wizara ya Afya kupatia kipaumbele deni kwa sababu hospitali zetu tayari zimeathirika vibaya na kucheleweshewa malipo. Jijini Nakuru, kwa mfano, tunaona bidhaa zinazozidi kuwasilishwa lakini tunabeba mzigo kwa sababu hatupati malipo,” alisema Gavana Kihika.

Wizara ya Afya (MoH) na Baraza la Magavana (CoG) linaloongozwa na Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru, hapo mbeleni limekutana kujadili masuala yanayohusu madeni huku mchakato wa kuhamia SHIF ukiendelea.

Mikutano hiyo iliangazia masuala muhimu ambayo ni pamoja na madeni.

MoH na serikali za kaunti zimeafikiana vilevile kuendesha kampeni ya umma kuhusu usajili wa wanachama wanaojiunga na SHIF.

Pande hizo mbili zitaendelea kushirikiana ili kuhakikisha utekelezaji bora wa Mpango wa Afya kwa Wote (UHC).

Waliafikiana vilevile kuwa MoH itatumia mfumo na data inayotumika kwa sasa katika NHIF iliyovunjiliwa mbali, kabla ya kuzindua SHIF.