Habari za Kitaifa

Mwana wa Nyachae ashtakiwa kuhusu usimamizi wa kampuni ya familia

Na SAM KIPLAGAT November 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MWANA wa kiume wa waziri wa zamani Simeon Nyachae na washirika wake wawili wa kibiashara wameshtakiwa kuhusiana na usimamizi wa kampuni ya familia.

Katika kesi iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu, Michael Moragia Nyachae, ambaye baba yake alifariki mwaka wa 2021, ameshtakiwa pamoja na Bw Aminmohamed Shamsudin na Bw Moez Ismael Jamal, kuhusu usimamizi wa kampuni ya Associated Auto Centre.

Eureka Holdings, iliyo na hisa katika Associated Auto Center pamoja na AJS Investments na Associated Motors, imewashtaki watatu hao, ikitaka wazuiwe kuwa wakurugenzi wa kampuni hiyo. Inadai kwamba kuendelea kwao kushikilia afisi kunaweza kudhuru kampuni ikiwa ni pamoja na kupotea kwa kifedha na usimamizi mbaya.

Kupitia wakili George Ouma, kampuni ya Eureka Holdings pia inataka agizo la mahakama ya kufunga akaunti kadhaa za benki, hisa na mali iliyosajiliwa kwa majina ya wakurugenzi hao watatu kusubiri kuamuliwa kwa kesi hiyo.

Zaidi ya hayo, kampuni inaomba agizo la kutafuta na kupata taarifa na rekodi za fedha za miaka kumi iliyopita za Associated Auto Center kutoka kwa katibu wa kampuni.

‘Mlalamishi anataka kupata taarifa na rekodi za [kampuni] kutoka mwaka wa 2014 ili kushiriki kikamilifu katika kesi na kulinda maslahi yake,’ wakili huyo anasema katika kesi hiyo.

Stakabadhi za mahakama zinaeleza kuwa wakurugenzi hao watatu wa Associated Auto wamekosa kulipa mikopo waliyokopa kutoka benki za Diamond Trust , Credit Bank Limited na Sidian Bank Limited.

‘Ni dhahiri kwamba kutochukua hatua kwa [wakurugenzi hao watatu] kunadhuru [Associated Auto Centre] na thamani ya mwenyehisa mlalamishi,” wakili huyo anasema kesi.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA