Naibu Msemaji wa serikali Chidzuga amtaka Rais Ruto kurejesha Mvurya na Jumwa kazini
NAIBU msemaji wa serikali Mwanaisha Chidzuga amemtaka Rais William Ruto kuwarejesha kazini mawaziri wa Pwani waliokuwa wakihudumu katika baraza lake alilovunjilia mbali siku chache zilizopita.
Akizungumza baada ya kuzindua shughuli ya ugavi wa chakula cha msaada kwa wakazi wa Kaunti ya Kwale katika eneo la Tsimba Golini, Bi Chidzuga alisisitiza haja ya viongozi zaidi kutoka Pwani kujumuishwa katika baraza jipya la mawaziri.
Haya yanajiri baada ya aliyekuwa Waziri wa Madini Salim Mvurya na mwenzake wa Masuala ya Jinsia na Utamaduni Aisha Jumwa kutemwa nje ya baraza hilo chini ya muda wa miaka miwili.
“Sisi kama Wapwani, alikuwa ametupatia mawaziri wawili, lakini tunaomba katika baraza jipya, aturejeshee hata zaidi ya mawaziri wawili. Hao waliokuwa walitekeleza majukumu yao vyema na ni ishara kuwa wapwani tunaweza,” Bi Chidzuga alisema.
Haya yanajitokeza naibu msemaji huyo wa serikali akiendeleza kampeni kuhimiza wakazi wa Kwale kujisajili na Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) katika maeneo ya Lungalunga, Matuga na Kinango.
“Nimechukua fursa ya kuwasajili wananchi ili Oktoba itakapofika wasiwachwe nyuma,” Bi Chidzuga alisema akiwarai wananchi kufika katika ofisi za huduma za serikali ili kujisajili.
Alisema ikiwa yeyote hana kitambulisho, atasajiliwa kwenye akaunti ya mzazi wake.
Bi Chidzuga aliongeza kuwa bima hiyo itakuwa na manufaa kwa akina mama ambao watapata matibabu baada ya kujisajili na bima hiyo.
“Wale ambao hawajiwezi, serikali itawapa matibabu ya bure bora tu umejisajili,” Bi Chidzuga alisema.
Usajili huo unaendelea licha ya Mahakama Kuu kutangaza Sheria tatu ambazo UHC ingetekeleza kuwa kinyume na sheria.
Majaji watatu walitangaza Sheria ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIA) 2023, Sheria ya Afya ya Msingi 2023 na Sheria ya Afya ya Kidijitali 2023, ambayo ilichukua nafasi ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF) kuwa batili.