Habari za Kitaifa

Ndio, nilipata D- lakini hivi karibuni nitaitwa Dkt Joho baada ya kupata PhD

Na CHARLES WASONGA August 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI Mteule wa Uchumi wa Maji, Uchimbaji wa Madini na Rasilimali za Majini Ali Hassan Joho amekiri kuwa alipata gredi ya D- katika mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) lakini hiyo haijamzuia kupata shahada ya uzamili.

Akipuuzilia madai kuwa hana shahada halali ya digrii akieleza mnamo 2008 alihitimu kwa shahaha ya digrii katika Chuo Kikuu cha Kampala.

“Baada ya hapo nilisomea shahada ya digrii katika taaluma ya Usimamizi wa Biashara katika Chuo Kuu cha Gretsa iliyoko Thika Kaunti ya Kiambu. Baada ya hapo nilisomea Shahada ya Digrii ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha ‘Harvard Kennedy School of Government Executive Education na nikafuzu,” Bw Joho akaambia Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi akipigwa msasa kubaini ufaafu wake kuhudumu kama Waziri Serikalini.

“Ndio nilipata gredi ya D- katika mtihani wa KCSE. Lakini sikuvunjika moyo, niliweza kuendelea kukwea ngazi ya masomo na sasa niko na shahadi za uzamili kutoka chuo kikuu chenye hadhi ya juu zaidi duniani,” Bw Joho akaiambia kamati hiyo.

Alikuwa akijibu maswali kutoka kwa kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah na kiranja wa wachache Junet Mohamed kuhusu suala la uhalali wa elimu yake.

Bw Joho alieleza kuwa wale wanaotilisha shaka uhalali wa masomo yake ni maadui wake wa kisiasa “wakiongozwa na Mzee mmoja wa Mombasa mwenye umri wa miaka 82.”

“Lakini Mheshimiwa Spika nataka kuihakikishia kamati hii kwamba endapo nitarejea hapa tena kupigwa msasa nitakuwa nimepata shahada ya uzamifu (PhD) na nitakuwa natambuliwa kama Dkt Joho,” akaiambia kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.

Gavana huyo wa zamani wa Mombasa alisema kuwa alitiwe shime na moyo katika safari ya kimasomo na msomi mashuhuri Profesa Ali Mazrui ambaye hakufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne “lakini hiyo haikumzuia kuendelea kimasomo hadi kuwa Profesa wa taadhima kubwa”.