Omtatah: Muafaka wa Raila, Ruto ni haramu
SENETA wa Busia, Okiya Omtatah, ameshutumu muafaka kati ya Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga, akisema hauzingatii Katiba na unasaliti imani ya mamilioni ya Wakenya.
Bw Omtatah alilinganisha muafaka huo na mapinduzi dhidi ya raia na Katiba, akisema viongozi hao wanalenga kubadili mfumo wa utawala ili kujinufaisha kibinafsi.
Alisema serikali jumuishi ambayo inapigiwa upato na wanasiasa hao wawili pia ni haramu kikatiba.
Seneta huyo amekuwa mkosoaji mkubwa kwa serikali na amewataka vijana wajisajili kwa wingi kama wapigakura ili kuweka uongozi mpya mamlakani mnamo 2027.
“Nawaomba Wakenya wajisajili kama wapigakura na waondoe Raila na Ruto madarakani 2027. Kile tunahitaji si serikali jumuishi bali sheria kuheshimiwa,” akasema.
Alikuwa akizungumza Jumatatu, Machi 17, 2025 kwenye kipindi cha asubuhi cha ‘Fixing The Nation’ katika runinga ya NTV na idhaa ya Nation FM.
Pia, seneta huyo ametaka Hazina Kuu Kifedha iondolewe kutoka kwa Wizara ya Fedha ili kuzuia rais kudhibiti rasilimali za nchi.
“Rais ameiteka hazina kuu na hakuna kinachofanyika bila idhini yake. Kama anataka bajeti, inastahili kupitishwa na bunge lakini sasa anafanya kile anachotaka,” akasema.
Kauli yake imekuja wiki mbili baada ya Rais na Bw Odinga kutia saini muafaka wa maelewano katika jumba la KICC.
Wawili hao walisema makubaliano hayo yalilenga kutuliza joto la kisiasa nchini hadi 2027.
Hata hivyo, Bw Omtatah alisema rais mwenyewe ana mamlaka ya kutekeleza Katiba bila kushauriana na Bw Odinga huku akiwataka Wakenya wote wapinge utawala wa sasa ambao unalemaza upinzani.
Alipinga kutekelezwa kwa Ripoti ya Kamati ya Maridhiano maarufu kama NADCO huku akipendekeza Katiba ifanyiwe marekebisho kuondoa mapungufu ambayo yapo.