Onyo: Baridi kali itaendelea katika maeneo haya kwa siku tano zijazo
Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya imewataka wakazi wa Nairobi kujiandaa kwa asubuhi za baridi, hali ya mawingu na vipindi vya mvua wikendi hii, baada ya kutangaza kuwa maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kupata mvua, hali ya baridi na upepo mkali kuanzia Agosti 22 hadi Agosti 25, 2025.
Katika utabiri wake, idara hiyo ilieleza kuwa mvua inatarajiwa kunyesha katika maeneo ya Nyanda za Juu mashariki na magharibi mwa Bonde la Ufa, eneo la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa na sehemu za kaskazini-magharibi mwa Kenya.
Idara hiyo ilisema kuwa kaunti kama Kisumu, Nakuru, Kakamega, Kericho na Bungoma zitapata mvua na radi nyakati za mchana, na viwango vya juu vya joto vikitarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 27 hadi 29 kwa kipimo cha selisias.
Katika maeneo ya kaskazini-magharibi mwa nchi kama vile Turkana na Samburu, mvua za hapa na pale na radi zinatarajiwa, japo kutakuwa pia na vipindi vya jua.
Joto la mchana katika kaunti hizo linatarajiwa kuwa kati ya nyusi joto 31 hadi 33 , huku joto la usiku likishuka hadi kati ya nyusi joto 9 hadi 13
Wakazi wa Nyanda za Juu mashariki mwa Bonde la Ufa, wakiwemo wa Nairobi, Nyeri, Kiambu na Meru, wametakiwa kujiandaa kwa asubuhi yenye baridi, mawingu na mvua za hapa na pale. Viwango vya juu vya joto vitakuwa kati ya nyusi joto 24 hadi 26, huku usiku ukitarajiwa kuwa na baridi kali ya kati ya nyusi joto 7 hadi 11.
Idara hiyo iliongeza kuwa maeneo ya kaskazini-mashariki kama Mandera, Garissa, Wajir, Marsabit na Isiolo yatakuwa na vipindi vya jua kwa kiasi kikubwa, huku mvua za hapa na pale zikitarajiwa kuanzia Jumapili. Maeneo haya pia yatakumbwa na joto kali, hadi kufikia nyusi joto 37wakati wa mchana, na kushuka hadi kati ya 14 hadi 16 usiku.
Katika maeneo ya chini kusini-mashariki, kama vile Machakos, Kitui, Makueni, Kajiado na Taita Taveta, asubuhi zitakuwa na mawingu kabla ya kugeuka kuwa jua, huku mvua nyepesi zikitarajiwa Jumapili. Joto la mchana litasalia kati ya nyusi joto 28 hadi 30.
Kwa kaunti za Mombasa, Kilifi, Kwale na Lamu, mvua inatarajiwa kunyesha asubuhi na jioni, huku vipindi vya jua vikishuhudiwa wakati wa mchana. Joto litasalia kuwa la wastani wa nyusi joto 29 hadi 30 mchana na kati ya 21 hadi 22 usiku.
Idara hiyo pia ilitoa onyo kwa maeneo ya Pwani, maeneo ya chini kusini-mashariki, kaskazini-mashariki na kaskazini-magharibi ya Kenya kwamba yatakumbwa na upepo mkali.
Upepo kutoka kusini hadi kusini-mashariki unaozidi kasi ya mafundo 25 unatarajiwa kuvuma katika maeneo ya pwani, na maeneo ya chini kusini-mashariki, kaskazini-mashariki na kaskazini-magharibi.
Wakazi wametakiwa kufuatilia taarifa kutoka kwa ofisi za hali ya hewa za kaunti na kuchukua tahadhari zinazofaa, hasa wale wanaoishi katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko.