Habari za Kitaifa

Oparanya agonganisha DPP na EACC katika juhudi za kunusuru uteuzi wake serikalini

Na SAM KIPLAGAT August 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KUONDOLEWA kwa mashtaka ya ufisadi dhidi ya aliyekuwa gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya kumezua mzozo mpya kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Ingawa tume ya kupambana na ufisadi ilishikilia kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuendeleza mashtaka ya mgongano wa kimaslahi na ufujaji wa pesa dhidi ya Bw Oparanya, Bw Ingonga alikuwa na maoni kwamba ingekuwa vigumu kumpata na hatia katika kesi hiyo kwa kukosa ushahidi wa kutosha.

Tume ya EACC ilishikilia katika barua iliyomwandikia Bw Ingonga mnamo Julai 31 kwamba stakabadhi na ushahidi uliowasilishwa kwake unaonyesha kuwa pesa zinazodaiwa kutumwa kwa akaunti ya kibinafsi ya Bw Oparanya na kwa mawakili wake zilikuwa ni ufisadi kutoka kwa wanakandarasi waliopewa zabuni mbalimbali na serikali ya Kaunti ya Kakamega.

“Kulikuwa na kesi ya wazi ya ulanguzi wa fedha na mgongano wa maslahi ambayo washukiwa hawawezi kutoa utetezi wowote dhidi yao. Kwa hivyo, tume inaamini kwamba ushahidi uliopatikana na uliowasilishwa kwa afisi yako unatosha na unaweza kuthibitisha kesi bila shaka yoyote,” barua ya Twalib Mbarak, Afisa Mkuu mtendaji wa EACC ilisema.

Bw Oparanya alitakiwa kushtakiwa kwa makosa 11 yanayohusiana na ufisadi kutokana na zabuni zilizotolewa kwa kampuni mbalimbali akiwa mkuu wa kaunti ya Kakamega.

Alipaswa kushtakiwa kwa mgongano wa maslahi na kupokea faida, kwa kununua mali anayomiliki.

EACC ilisema uchunguzi ulibaini kuwa Bw Oparanya alidaiwa kupokea kimakosa Sh56.7 milioni kutoka kwa serikali ya kaunti ya Kakamega.

Awali Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma alikubaliana na mapendekezo ya EACC ya kumshtaki Bw Oparanya lakini akafanya mabadiliko mnamo Julai, kufuatia ombi la Bw Oparanya kupitia kwa mawakili wake.

Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya EACC kuliandikia Bunge kuhusu hali ya kesi hiyo huku wakili wa Bw Oparanya akisema barua ilikuwa na nia mbaya.

Bw Oparanya ni miongoni mwa mawaziri wateule ambao wanapigwa msasa kuhusu ufaafu wao kuhudumu serikalini na maswali kuhusu ufisadi yanatarajiwa kuibuliwa atakapofika mbele ya kamati ya Bunge Jumapili.

Wakili wa Bw Oparanya Dkt Ken Nyaundi alisema kwamba walimwandikia DPP mnamo Julai 24, 2024 wakimuomba apitie uamuzi wa kumshtaki baada ya kupata ushahidi mpya, kuonyesha kwamba pesa zinazodaiwa kulipwa kwa akaunti ya Bw Oparanya zilikuwa za mkopo.

Dkt Nyandi alisema EACC ilipokea mawasiliano kutoka kwa DPP na uamuzi wa kutupilia mbali uamuzi wa kumfungulia mashtaka Bw Oparanya, EACC iliandikia Bunge ikipuuza mawasiliano muhimu ambayo yalitangulia barua yao.

“Hakuwezi kuwa na chuki kubwa zaidi kuliko hii,” Dkt Nyaundi alisema.

Aliongeza, “Tunaagizwa kuwajulisha kuwa hakuna upelelezi wala mashtaka yanayomkabili Bw Oparanya kustahili malalamishi dhidi yake.”

Inafaa kukumbuka kuwa kwa msingi wa barua ya DPP na baada ya kupokea barua hiyo hiyo, EACC inafaa kutambua kwamba madai yote ya makosa kutoka kwa Bw Oparanya yalikataliwa.

Kwa kukubaliana na Bw Oparanya, DPP alibainisha kuwa pesa hizo ni mkopo.

Mashtaka yaliyopendekezwa yalitokana na pesa alizolipwa na Mkurugenzi wa Sabema International Ltd na Sesela Resources Ltd, Joseph Obulunji Okutoyi kwa kampuni ya Marende & Nyaundi Company Advocates ili kumwezesha gavana huyo wa zamani kununua nyumba huko Karen.

Sesela Resources Ltd ilishirikiana na serikali ya kaunti ya Kakamega kwa ujenzi wa Barabara ya Tsalwa Junction-Ombwaro-Manyulia kwa gharama ya Sh216 milioni.

Baada ya kulipwa Sh35.8 milioni, mwanakandarasi alihamisha Sh10 milioni kwa mawakili wa Oparanya.