Pigo tena kwa Gachagua mahakama ikikataa kutoa amri kesi zikifika 19
JUHUDI mpya za kuzuia kung’olewa mamlakani kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua Jumatatu zilipata pigo katika Mahakama Kuu.
Jaji Bahati Mwamuye aliamrisha kuwa kesi ambayo iliwasilishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala ipelekwe kwa Jaji Eric Ogola. Ni Jaji Ogola atasikiza kesi zote zilizowasilishwa na watu mbalimbali wakipinga kutimuliwa kwa Naibu Rais.
Kupitia wakili Mwenda Njagi, Bw Malala aliwasilisha kesi hiyo ambayo haitakuwa na mashiko ikizingatiwa hoja ya kumtimua Naibu Rais itawasilishwa bungeni mnamo Jumanne.
Wakili huyo jana alisema kesi hiyo haitakuwa na maana iwapo amri ambayo waliitaka itolewe haingetolewa kwa kuwa hoja itakuwa ishajadiliwa na uamuzi kutolewa.
“Mahakama hii imetambua kuwa kuna kesi kadhaa kuhusiana na kuondolewa mamlakani kwa Naibu Rais na inaona heri kesi hizo ziunganishwe. Naomba kesi hii ipelekwe kwa Jaji Ogola iunganishwe na nyingine na mahakama inakataa kutoa amri za muda,” akasema jaji huyo.
Kupitia wakili Paul Nyamodi, Bunge jana lilifichua kuwa kuna kesi 19 ambazo zimewasilishwa mahakamani kupinga kutimuliwa kwa Bw Gachagua.
Wakili huyo alisema kuwa ili kesi hizo zisikizwe kwa rahisi na haki itolewe, kuna haja ya kuunganishwa pamoja badala ya kusikizwa moja baada ya nyingine.
“Amri kuhusu kuunganishwa kwa kesi hizo itazuia mahakama kuwa na vikao tofauti kusikiza kesi moja. Ikifanyika hivyo, korti inaweza kuafikia uamuzi ambao unagongana na kuaibisha mahakama,” akasema Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge.
Ombi la kuunganishwa kwa kesi hizo na kusikizwa kisha kuamuliwa pamoja pia lilikubaliwa na Seneti.
Katika kesi yake, Bw Malala anasema kuwa Bunge la Kitaifa jinsi lilivyo halitimizi vigezo vya kikatiba kutokana na kukosa kutimiza usawa wa jinsia.
Kando na Bw Malala, Naibu Rais mwenyewe amefika kortini kupinga kutimuliwa kwake akisema kuwa madai yanayotumiwa kumsulubisha hayana mashiko.
Pia Bw Gachagua amesema kuwa mikutano ya ushirikishaji wa umma ambayo ilifanyika wikendi haitoshi kubadilisha uamuzi wa raia ambao walimpigia kura pamoja na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu uliopita.
“Hoja ya kunitimua inalenga kubadilisha uamuzi wa Wakenya wengi ambao walinipigia kura kuwa Naibu Rais wa Kenya. Madai yaliyowekwa dhidi ya yangu ni ya uongo na hayana msingi hivyo basi hayatimizi vigezo vya kung’atuliwa kwangu,” akasema kwenye kesi yake.