Habari za Kitaifa

Raila asihi vijana wasichoke kupigania uongozi bora wa nchi yao

Na STEPHEN MUNYIRI July 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KINARA wa Azimio Raila Odinga jana aliwaongoza viongozi wengine wa kisiasa kuwahimiza vijana kuendelea na harakati zao za kukomboa nchi yao kiuchumi.

Haya yanajiri huku wanasiasa wakiwahimiza viongozi wa makanisa kuiga makasisi wa miaka ya zamani kama Kasisi Timothy Njoya kujiunga na Gen Z kuikomboa nchi.

Viongozi hao waliohudhuria mazishi ya mwanasiasa mkongwe Maina Wanjigi katika Kaunti ya Nyeri, walisema kuibuka ghafla kwa Gen Z nchini ni “kazi ya Mungu” na kuongeza kuwa Wakenya wana fursa ya mwisho ya kuikomboa nchi kutoka kwa utawala mbaya.

Waliohudhuria hafla hiyo pamoja na Bw Odinga ni Gavana James Orengo, Gavana Mutahi Kahiga, kiongozi wa chama cha Roots George Wajakoyah, Katibu mkuu wa chama cha Jubilee Jeremiah Kioni, aliyekuwa Mbunge wa Starehe Maina Kamanda miongoni mwa wengine.

Bw Odinga aliwasifu vijana kwa ujasiri wao wa kusimama dhidi ya utawala wa Rais William Ruto akisema Wakenya wanatamani mabadiliko na atawaunga mkono.

“Gen Z walipoanza maandamano waliniomba nitulie.Najivunia wao na nataka niwahakikishie hata nikitulia ninawaunga mkono. Najua wamekunywa vitoa machozi lakini wacha niwaambie haitakuwa rahisi kwa sababu tumeshaonja vitoa machozi hapo awali. Msilegee hadi mrejeshe utawala bora katika nchi hii,” alisema.

Bw Odinga aliongeza, “Kenya inahitaji mazungumzo ya dhati kujadili suala la ufisadi, ukabila na upendeleo, ukosefu wa ajira kwa vijana, ukatili wa polisi kwa watu wasio na hatia.”

Alitoa changamoto kwa viongozi wa makanisa kuungana na Gen Z na Wakenya wengine katika harakati za kurejesha utawala bora.

“Kanisa lazima lihubiri neno la Mungu na kusimama kidete na watoto wa Mungu, wanapaswa kuambia ukweli viongozi walio mamlakani,” alisema.

Gavana James Orengo alisema Gen Z walitumwa na Mungu kukomboa nchi akiwataka Wakenya kutumia nafasi hii kurudisha demokrasia na utawala bora.