Habari za KitaifaMakala

Raila ni bingwa wa miungano na mafarakano

Na BENSON MATHEKA September 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

AZMA ya kinara wa ODM Raila Odinga ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) inaendeleza mtindo wake wa kubuni miungano mipya na wakati huo huo kuzua migawanyiko ya kisiasa nchini.

Azma hiyo imeunganisha mahasimu wa kisiasa ambao kwa miaka 13 iliyopita walikuwa wakitofautiana sana kisiasa.

Odinga mwenyewe alikuwa akitofautiana na Rais William Ruto huku wakirushiana maneno makali tangu kampeni za uchaguzi mkuu wa 2013 ambao Raila aligombea kwa muungano wa Coalition for Restoration of Democracy (CORD), mgombea mwenza wake akiwa kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka. Katika uchaguzi huo, Rais Ruto alikuwa mgombea mwenza wa Uhuru Kenyatta katika muungano wa Jubilee.

Baada ya Uhuru kushinda uchaguzi huo, Bw Odinga aliendelea kukosoa utawala wa Jubilee ambapo alilumbana vikali na Ruto aliyekuwa mtetezi shupavu wa Rais Uhuru Kenyatta.

Hali hii iliendelea katika uchaguzi mkuu wa 2017 ambao Bw Raila na Musyoka waligombea chini ya muungano wa NASA na kubwagwa na Uhuru na Ruto waliopeperusha bendera ya chama cha Jubilee.

Katika uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Raila na Ruto walikuwa kama stima na maji wakishindana kupitia miungano ya Azimio la Umoja One Kenya na Kenya Kwanza mtawalia.

Bw Raila alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Ruto naye Kiongozi wa Nchi akiapa kutoshirikisha upinzani katika serikali yake.

“Wasahau nusu mkate na kufanya kazi yao ya upinzani. Hii ni serikali ya mahasla,” Rais Ruto alinukuliwa akisema mara si moja.

Washirika wa Bw Raila katika Azimio, walikuwa Martha Karua wa Narc Kenya aliyekuwa mgombea mwenza wake, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Uhuru Kenyatta wa Jubilee, Eugene Wamalwa wa DAP- Kenya na Peter Munya wa PNU miongoni mwa wengine huku wale wa Rais Ruto katika Kenya Kwanza wakiwa naibu wake Rigathi Gachagua katika chama cha UDA, Bw Musalia Mudavadi wa ANC na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya miongoni mwa wengine.

“Kwa wakati huu Rais Ruto anaungana na Bw Odinga kwa wadhifa wa AUC, naye waziri mkuu huyo wa zamani akiunga serikali ya Kenya Kwanza.

“Hii imezua tofauti za wazi kati ya Bw Odinga na washirika wake katika Azimio akiwemo Bw Uhuru, Bi Karua na Bw Musyoka huku nia ya kiongozi huyo wa ODM ikionekana kusambaratisha muungano huo wa upinzani, hatua itakayompa Ruto mteremko katika utawala wake,” akasema mdadisi wa siasa Beatrice Waithera.

Anasema ukuruba wa kisiasa kati ya Rais Ruto na Raila umesukwa kuzua migawanyiko zaidi ya kisiasa ikizingatiwa kuwa siasa za Kenya zimekitwa katika ukabila na maeneo. Sio siri kwamba ODM ina wafuasi wengi Nyanza na Magharibi na sehemu za Pwani.

Huko ndiko viongozi wa ODM walioteuliwa mawaziri walitoka katika kile kilichotajwa kama Serikali Jumuishi. Hii iliacha ngome za vyama vingine tanzu za Azimio zikiwa zimetengwa na lengo hapa lilikuwa ni kusambaratisha upinzani,” aongeza Waithera.

Rais Ruto aliteua waliokuwa manaibu wa Raila katika ODM, Hassan Joho na Wycliffe Oparanya, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi na aliyekuwa kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi kuwa mawaziri.

Kulingana na mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, japo azma ya Raila inaonekana kuungwa na viongozi tofauti ndani na nje ya serikali, inazua mwelekeo wa kisiasa ambao unagawanya nchi.

“Kinachofanya vigogo wa kisiasa kuunga azma ya Raila AUC ni kuwa ataondoka katika siasa za Kenya iwapo atashinda.

Pili, inazua migawanyiko ndani ya muungano tawala na upinzan56i. Tayari kuna tofauti zinazofunikwa kati ya Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua huku zinazokumba Azimio zikionekana wazi,’ akasema Dkt Gichuki.

Anasema japo sio jambo geni kwa miungano ya kisiasa kuvunjika, azma ya Raila kuwania uenyekiti wa AUC inazua mwamko na mwelekeo mpya wa kisiasa nchini.

“Raila ni bingwa wa kuunganisha na shupavu wa kuzua migawanyiko kutimiza maslahi yake. Alivunja Cord, akavunja Nasa, sasa analenga Azimio na anaokenana kufaulu. Mwaka wa 2001 nusura avunje Kanu lakini akafaulu kuififisha,” asema Gichuki.