Rais asema hakuna cha Wakenya kuvalia viatu kutoka nje
NA CHARLES WASONGA
RAIS William Ruto ametangaza serikali itawekeza Sh100 milioni katika kiwanda cha kutengeneza viatu na ifikapo mwaka wa 2027, Kenya itakoma kuagiza viatu kutoka nje.
Akiongea Jumamosi mjini Bungoma wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Madaraka Dei, Dkt Ruto alisema kiwanda hicho kitachangia ongezeko la uzalishaji wa vyatu nchini kutoka viatu jozi milioni nane hadi jozi 36 milioni, kufikia thamani ya Sh76 bilioni kwa mwaka.
“Hii itahakikisha kuwa taifa letu linajitosheleza kwa viatu kiasi kwamba ifikapo mwaka wa 2027 tutakoma kuagiza viatu kutoka nje. Aidha, kiwanda hicho kitakachojengwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Ustawi wa Eneo la Kusini mwa Ewaso Ng’iro (ENSDA) kitatoa ajira ya hadi 100,000 kutokana nafasi 17,000 zilizoko sasa katika sekta hiyo ya viatu,” akasema.
“Narudia hapa kwamba baada ya kiwanda hicho kuanza kazi, hatutakuwa tukiagiza viatu kutoka ng’ambo. Tutakuwa tukivalia vyatu vyetu, vilivyotengezwa nchini Kenya kwa kutumia ngozi yetu,” Dk Ruto akasisitiza.
Aidha, alisema kuwa kiwanda hicho kitatengeneza bidhaa zingine za ngozi kama vile mishipi, vibeti na mikoba.