Habari za Kitaifa

Ruto alivyoibuka sungura mjanja kwa kumbebesha Raila zigo la serikali yake

Na COLLINS OMULO July 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ameonekana kuerevuka na kusukuma zigo zito la serikali yake kwa Kinara wa ODM Raila Odinga baada ya kuwateua wandani wake kwenye wizara muhimu zinazokabiliwa na matatizo chungu nzima.

Kiongozi wa nchi aliwateua mbunge wa mteule John Mbadi kama waziri wa fedha, Opiyo Wandayi Kawi, Wycliffe Oparanya (vyama vya ushirika) na Hassan Joho (madini na uchumi samawati).

Hata hivyo, Bw Mbadi, Oparanya na Wandayi watakuwa wanashikilia wizara ambazo zimechangia Kenya Kwanza kukabiliwa na maasi nchini. Kuwapa wandani wa Raila wizara hizo kunaonekana kama kuwekea kiongozi huyo wa upinzani mtego kwa sababu wakikosa kufaulu, basi Raila ndiye atakuwa pabaya.

Bw Mbadi atakuwa akichukua usukani wakati ambapo Wakenya wamelalamikia sera ya Kenya Kwanza kuwaongezea ushuru. Ni ushuru huo mwingi ndio ulisababisha maandamano nchini na kusababisha Rais Ruto kuondoa Mswada wa Fedha 2024/25.

Mwenyekiti huyo wa ODM atakuwa anasimamia wizara hiyo inayotarajia kugeuza dhana kuwa serikali hii imejikita tu katika kuwaongezea Wakenya ushuru ilhali maendeleo hamno.

Pia atalazimika kuibuka na sera za kubana matumizi ya serikali baada ya mswada wa fedha kuondolewa. Tayari baadhi ya Wakenya wanamtaka Bw Mbadi aondoe ushuru wa nyumba ambao aliupinga vikali kwenye majukwaa mbalimbali kabla ya uteuzi wake.

Bw Oparanya naye atasimamia wizara ambayo inahusika na Hazina ya Hasla ambayo imekashifiwa sana na Wakenya. Rais Ruto alizindua hazina hiyo ya Sh50 bilioni mnamo 2022.

Rais wakati wa kampeni aliahidi kuwa hazina hiyo ingewakwamua Wakenya wengi hasa wafanyabiashara wadogo wadogo ila imekuwa ikikabiliwa na changamoto tele baadhi ya watu wakishindwa kupata mkopo huo.

“Iwapo Rais atafeli basi 2027 ikifika, atasema kuwa ni Raila na wandani wake ndio walimwaangusha kwa kuwa aliwatunuku wizara muhimu. Ukisimamia hazina ya Hasla na pia wizara ya fedha basi una ufunguo wa ufanisi wa utawala huu,” akasema Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Javas Bigambo.

Wakenya wamekuwa wakilalamikia kupotea kwa umeme mara kwa mara hali ambayo inatatiza shughuli zao. Hilo likifanyika, basi atakayekuwa akilaumiwa ni Bw Wandayi.

Miundomsing nzee, ufisadi, umeme kuunganishwa kwa njia ya ukora na kupanda kwa gharama ya umeme ni kati ya changamoto ambazo zinamsubiri mbunge huyo wa Ugunja azitatue.