Ruto apiga marufuku watumishi wa umma kushiriki harambee
RAIS William Ruto amepiga marufuku harambee ambazo wanasiasa wamekuwa wakitumia kujipigia debe.
Rais amemwagiza Mwanasheria Mkuu Justin Muturi kutayarisha sheria na kuunda utaratibu wa michango ya wazi kwa lengo la kutoa misaada hasa kwa matibabu.
“Naagiza Mwanasheria Mkuu kuandaa na kuwasilisha sheria kufafanua utaratibu uliopangwa na wa uwazi wa michango ya umma,” alisema.
Kwa kufanya hivyo, alipiga marufuku watumishi wa umma kushiriki katika harambee.
“Hakuna afisa wa serikali atakayehitajika kushiriki katika kuchangisha pesa za umma katika harambee,” Rais Ruto alisema.
Maafisa wa serikali na watumishi wa umma wamekuwa wakimulikwa kutoa mamilioni ya pesa makanisani na hafla mbalimbali za kuchangisha pesa wakati ambapo serikali iaendelea kutoza ushuru wa juu ili kuendeleza shughuli za serikali.
Rais Ruto alidokeza kuwa atafanyia mabadiliko serikali yake wakati wowote.