Sababu za mali ya Moses Kuria kunadiwa kulipa Benki ya Equity mkopo wa mamilioni
MALI ya mshauri mkuu wa Rais William Ruto, masuala ya kibiashara na uchumi, Moses Kuria itauzwa wakati wowote sasa na Benki ya Equity baada ya Mahakama kuu kukataa kusitisha hatua ya kunadi mali ya waziri huyo wa zamani.
Benki hiyo ya Equity inamdai Kuria mkopo wa Sh54 milioni aliochukua kustawisha shamba lake lililoko Kiambaa, Kaunti ya Kiambu.
Jaji Aleem Visram wa Mahakama Kuu Milimani alisema Kuria alishindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuwezesha korti kuzima madalali wasiuze mali ya mshauri huyo wa rais.
Jaji Visram alisema Benki ya Equity imefuata sheria ipasavyo kupata pesa ilizomkopesha Kuria.
Jaji alisema jitihada za benki hiyo ziligonga mwamba.
Mahakama ilisema Kuria amekiri kwamba alipokea mkopo kutoka kwa benki hiyo na hajaulipa.
Ameungama kwamba mkopo huo amekawia muda mrefu kabla ya kuulipa.
“Jitihada za Kuria kubadilishiwa masharti ya kulipa mkopo huo zimegonga mwamba. Muda mwingi umepita na sasa benki haina budi ila kuuza kwa njia ya mnada mali ya Kuria,” Jaji Visram alisema.
“Hakuna njia benki hii itazuiliwa kutekeleza majukumu yake kuuza kwa njia ya mnada mali ya Kuria kujilipa mkopo ambao umezidi Sh54 milioni,” Jaji Visram alisema.
Mshauri huyo wa rais aliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu kuzima kampuni ya madalali ya Garam Investments Auctioneers isiuze mali yake kutokana na mkopo huo wa Benki ya Equity wa Sh54 milioni.
Benki hiyo sasa iko huru kuuza shamba la Kuria lililoko Kiambaa, Kiambu.
Mahakama ilifahamishwa na Benki ya Equity kwamba waziri huyo wa zamani wa Uwekezaji na Biashara alipokea mkopo wa Sh54 milioni mnamo Machi 15, 2018 kujenga maghorofa kwenye mashamba yake mawili.
Kuria aliafikiana na Benki kwamba ataanza kulipa mkopo huo baada ya miezi tisa baada ya kuupokea.
Ushahidi ulionyesha Kuria aliahidi kulipa mkopo huo kwa mara 111.
Kila wakati aliahidi kulipa Sh402, 832 hadi aukamilishe.
Jaji Visram alisema ushahidi unaonyesha kwamba Kuria alishindwa kulipa mkopo huo.
Januari 24, 2025, Bw Kuria aliahidi kuulipa kwa kiwango cha Sh850, 000 kwa mwezi lakini pia akashindwa.
Kuria alieleza mahakama kwamba alikuwa amelipa Sh733, 000.
Hata hivyo, Jaji Visram alisema licha ya Kuria kuugua na kulazwa hospitalini ng’ambo kati ya 2020 na 2021, ugonjwa si sababu mwafaka kushawishi mahakama kuzima uuzwaji wa mali yake.