Habari za Kitaifa

Ruto, Museveni wamshangaa mwenzao wa Tanzania kuongeza vikwazo vya biashara

Na KEVIN CHERUIYOT July 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto na Rais wa Uganda Yoweri Museveni wametangaza kwa pamoja kwamba vizingiti vya kibiashara kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) vinaathiri maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.

Wakizungumza kwa pamoja katika Ikulu ya Nairobi siku ya Jumatano, viongozi hao wawili walieleza wasiwasi wao kuhusu baadhi ya mataifa kukataa kufungua masoko yao kwa nchi wanachama wenzao, hali ambayo imesababisha mzunguko wa vizuizi vinavyokwamisha biashara huru.

Viongozi hao walikutana kujadili masuala ya biashara, usalama na amani ya kikanda. Mkutano wao umefanyika wakati ambapo vizingiti visivyo vya ushuru vimeongezeka licha ya uwepo wa fursa kubwa ya biashara katika ukanda huu.

Rais Museveni alisema ukanda wa Afrika Mashariki unapaswa “kuamka” na kufanya maamuzi ya busara kuhusu biashara na uchumi. Alitarajiwa kutoa mhadhara wa hadhara katika Chuo cha Kitaifa cha Ulinzi (NDC), Nairobi.

Rais Ruto alisema walijadili kuhusu “vizingiti sugu visivyo vya ushuru vinavyokwamisha uhamishaji wa bidhaa na kudhoofisha malengo ya ujumuishaji wa kikanda chini ya mfumo wa EAC.”

Ingawa hawakutaja nchi mahsusi, mkutano huo umejiri baada ya Tanzania kuchafua mkataba wa soko la pamoja kwa kupiga marufuku wageni kushiriki katika shughuli 15 za kiuchumi zinazochukuliwa kama biashara ndogo. Tanzania ilisema ilikuwa ikiwalinda wananchi wake dhidi ya ushindani usio wa haki kutoka kwa wageni – japo raia wake wana fursa sawa katika mataifa mengine ya EAC.

Tanzania pia ilirudisha ushuru wa viwanda kwa bidhaa zinazozalishwa katika nchi wanachama, jambo linaloonekana kuvunja kanuni ya ushuru wa pamoja wa nje unaolenga kulinda ukanda huu na kuchochea ukuaji wa viwanda vyake.

Rais Museveni alisema ukanda wa Afrika Mashariki umejipanga kama nyumba iliyo na vyumba katika mataifa tofauti.

“Inaweza kuwa Uganda haina bahari. Sudan Kusini, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad…hata Ethiopia hiyo kubwa haina bahari. Na watu hawafanyi kazi kutatua hilo. Na wewe ni rais, au waziri…unaongoza nini?” alihoji katika mkutano huo wa pamoja.

“Ukiwa rais hauwezi kutatua suala la upatikanaji wa masoko…nani atanunua bidhaa zako? Ukikosa jibu la hilo na wewe ni kiongozi…hatima ni giza.”

“Unawezaje kuwa na sebule katika nchi moja, chumba cha kulala nchi nyingine, jikoni nchi nyingine…huu ni mipangilio gani hii?” aliendelea kuhoji.

Mkutano huo ndio wa kwanza mwaka huu baina ya viongozi hao wawili, huku Kenya na Uganda zikiwa na migogoro ya mara kwa mara kuhusu bidhaa kama maziwa na kuku.

“Tunaendelea kuona EAC kama mfano bora wa ujumuishaji wa kikanda. Tunasisitiza umuhimu wa umoja, mwelekeo wa kiuchumi wa pamoja na ustawi wa pamoja kama misingi ya maendeleo ya pamoja,” alisema Rais Ruto.

Kulingana na sekretarieti ya EAC, biashara ya ndani baina ya wanachama imekuwa ikiongezeka ingawa imekuwa ikitatizwa na vikwazo visivyo vya ushuru. Mnamo 2024, biashara ya jumla ya EAC na mataifa mengine ilikua kwa asilimia 14.17 hadi kufikia Dola za Amerika 124.9  bilioni kutoka 109.4 bilioni.