Habari za Kitaifa

Sababu za wahadhiri kusitisha mgomo

Na DAVID MUCHUNGUH, CHARLES WASONGA September 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MGOMO wa wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma na umefikia kikomo baada ya serikali kuelewana na viongozi wa vyama vya kutetea masilahi ya wafanyakazi hao.

Mgomo huo uliodumu kwa siku nane ulimalizika baada ya viongozi wa chama cha wahadhiri (UASU) na kile cha wanafanyakazi wasio wahadhiri (KUSU) kufanya mkutano na Waziri wa Leba Alfred Mutua jijini Nairobi na kufikia makubaliano.

Kulingana na makubaliano hayo, wanachama wa vyama hivyo watapata nyongeza ya kati ya asilimia saba na asilimia 10 ya mishahara yao.

Aidha, watapata nyongeza ya mishahara ya asilimia nne kila mwaka, moja kwa moja, ndani ya kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji wa Mkataba wa Maelewano (CBA) ya kuanzia Julai 1, 2023 hadi Juni 30, 2025.

Viongozi wa UASU pia waliafikiana na Waziri Mutua kuwa umri wa kustaafu kwa wahadhiri utakuwa miaka 70.

“Kwa sasa chama kimefutulia mbali mgomo wa wanachama wake ambao umedumu kwa siku nane, kufuatia maafikiano hayo. Kwa hivyo, mwajiri ataondoa, bila masharti, kesi nambari E780 iliyowasilishwa katika mahakama ya Leba na Masuala ya Uajiri,” chama cha Uasu kikasema kwenye taarifa.

Aidha, vyama vya UASU na KUSU vilikubaliana na Wizara ya Leba kwamba wanachama wao hawatachukuliwa hatua zozote za kinidhamu kwa kushiriki katika mgomo huo