Shirika la Femnet lahimiza elimu kamilifu kuhusu masuala ya kingono kwa vijana
SHIRIKA la kijamii limehimiza haja ya elimu kamilifu kuhusu masuala ya kingono hasa kwa vijana kuhakikisha kuwa wanawezeshwa kufanya maamuzi sahihi.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la The African Women’s Development and Communication Network (FEMNET) Bi Memory Kachambwa, ameeleza kuwa ingawaje kuna mjadala kuhusu ni habari zipi za kutoa kwa vijana, ni wakati mwafaka kwa masuala hayo kuangaziwa kwa kina.
Alisema hayo katika mahojiano na wanahabari wakati wa warsha ya siku tatu jijini Nairobi, na ambayo imeleta pamoja wawakilishi kutoka mataifa zaidi ya 15 barani Afrika kwa lengo la kuunda mfumo ambao utatoa mwelekeo kuhusiana na masuala ya kijinsia, afya ya uzazi na haki husika.
“Nadhani kwangu mimi hili ni suala kuu, kwa sababu kuna mijadala ya kila aina kuhusu ni kipi tunachofaa kufunza, ni aina gani ya habari zinazowafaa watu wachanga. Na baada ya kupata habari hizo, ni sera zipi ambazo zipo kuwalinda? Kwa hivyo, moja wapo ya mambo tunayosikia ni kuhusu umri unaofaa, lakini tunajua kuwa watu wetu wachanga tayari wanashiriki mambo haya katika umri mdogo,” anasema.
Bi Kachambwa anasema kuwa ingawaje upo wasiwasi mwingi kuhusu utoaji wa habari hizi, la muhimu zaidi ni kuhakikisha kuwa wanapata habari muhimu na za sahihi ili kuepuka nyingi potovu zilizopo kwa baadhi ya vyombo vya habari na mitandaoni.
“Tunahitaji elimu inayoshughulikia mambo yote, kwa sababu utaficha baadhi ya mambo, lakini mambo hayo, watoto watayapata na huenda wasiwe na suluhu wakiwa vyuoni za kuweza kuyatatua. Kwa hivyo, kwangu mimi, tunahitaji sera maalum na habari sahihi kuhakikisha wanawake na wasichana wetu wako salama,” anasema.
Shirika hilo linapanga kufanya mikutano na wazee wa kijamii, kidini miongoni mwa makundi mengine, kwa lengo la kuweza kuwa na mwelekeo kuhusiana na masuala ya haki za kijinsia na afya ya uzazi.
Wakati huo huo, Bi Kachambwa amehimiza haja ya kutenga fedha zaidi kukabili masuala ya ukeketaji wa wasichana hasa katika miji iliyopo mipakani, desturi potovu ambayo anasema iliongezeka sana wakati wa janga la Covid 19.
“Pia, tumeona ndoa za lazima na pia za watoto na hayo ni baadhi ya masuala yanayotutia hofu,” anasema akiongeza kuwa dhuluma dhidi ya wanawake na watoto na pia visa vya mauaji ya wasichana na wanawake ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa Kenya ni mambo yanaoibua wasiwasi.
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), haki hizi za masuala ya kijinsia na afya ya uzazi ni pamoja na ufikiaji wa mbinu za upangaji uzazi, matibabu ya uzazi, afya ya wajawazito, kupata tiba ya maradhi ya zinaa, kulindwa dhidi ya dhuluma za kijinsia, elimu ya mahusiano salama, miongoni mwa nyingine.
Pia inaeleza kuwa upataji wa huduma za afya ya uzazi ni haki za kibinadamu ambazo, lengo lake sio kuwa na afya iliyoimarika pekee, bali pia inachangia katika usawa wa kijinsia na maendeleo kwa jumla.