Habari za Kitaifa

Shule zataka wanafunzi wasalie nyumbani kwa hofu ya fujo Saba Saba

Na MERCY SIMIYU July 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHULE mbalimbali nchini zimetuma ujumbe kwa wazazi, zikiwashauri kutowapeleka watoto wao shuleni kesho, Julai 7, kutokana na hofu ya ghasia zinazotarajiwa wakati wa maadhimisho ya Saba Saba.

Wakuu wa taasisi hizo walitaja sababu za kiusalama kwa wanafunzi na walimu, wengi wakisema watasubiri hali itulie kabla ya kurejelea shughuli za kawaida.

Maandamano hayo, ambayo yamekuwa yakishika kasi katika miji mikuu nchini, yanatarajiwa Jumatatu, siku ya kumbukumbu ya maandamano ya kihistoria ya Saba Saba mnamo 1990 yaliyolenga mageuzi ya kidemokrasia nchini Kenya.

“Kwa sababu ya maandamano yanayotarajiwa siku ya Jumatatu 7/7/25, tunawaomba wanafunzi wabaki nyumbani na warudi shuleni Jumanne 8/7/25, kama kawaida. Asanteni,” ulisema ujumbe kutoka shule zaidi ya 10.

Hatua hii ya pamoja inajiri huku kukiwa na hofu kwamba, maandamano hayo yanayoopangwa na wanaharakati wa kizazi cha Gen Z pamoja na mashirika ya kijamii yanaweza kusababisha vurugu katika miji mikuu na barabara kuu.

Wadau wa elimu wameeleza wasiwasi wao kuhusu usumbufu unaoendelea kwa masomo kutokana na maandamano ya kitaifa, wakitaka serikali kuhakikisha usalama wa wanafunzi na walimu wakati wowote maandamano kama hayo yanapotokea.

Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Chama cha Wadau wa Elimu Kenya kilisema kuwa maandamano ya hivi majuzi, ambayo mara nyingi huandamana na vurugu na makabiliano ya kikatili kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama, yamesababisha hofu kubwa kwa wazazi na kusababisha kufungwa kwa shule kote nchini.

“Jana, wazazi walianza kupokea ujumbe mfupi kutoka kwa shule ukieleza kuwa watoto hawapaswi kuripoti shuleni Jumatatu Julai 7 2025 (Saba Saba) kutokana na maandamano yanayotarajiwa, ambayo wakati mwingine hugeuka kuwa vurugu na makabiliano ya kikatili kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama,” alisema Ndung’u Wangenye, Katibu Mkuu wa Chama cha Wadau wa Elimu Kenya.

“Wiki iliyopita, Jumatano Juni 25 2025, wazazi walipokea taarifa kama hiyo kutoka kwa shule mbalimbali,” aliongeza.Chama hicho kilionya kuwa, usumbufu wa mara kwa mara unahatarisha kalenda ya masomo ambayo tayari ni dhaifu, hasa wakati huu ambapo shule bado zinapambana kutekeleza mtaala wa Umilisi (CBC).

“Inapaswa kufahamika kuwa shule bado zinajaribu kujenga misingi imara ya utekelezaji wa CBC na usumbufu wa mara kwa mara wa shughuli za shule utaathiri kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa mtaala huu mpya,” alisema.

Aidha, alieleza kuwa sekta ya elimu bado haijapona kutokana na usumbufu wa awali kama vile kufungwa kwa shule kwa muda mrefu kutokana na janga la COVID-19 kati ya mwaka 2021 na 2022, migomo ya walimu hasa wanachama wa KUPPET mwaka jana, na mafuriko ya kitaifa yaliyoathiri maelfu ya wanafunzi.

Wadau sasa wanaitaka serikali kuweka mbele usalama na uendelevu wa elimu kwa kuhakikisha kuna ulinzi wa kutosha kwa shule wakati wa maandamano, na kuwalinda wale waliotaja kama ‘waathirika halisi’ wa vurugu hizi ambao ni watoto wa shule.Mnamo Juni 25, watu wasiopungua 16 walipoteza maisha na zaidi ya 400 kujeruhiwa.