Habari za Kitaifa

Si rahisi kwa Gachagua wazee wa Njuri Ncheke wakimtema

Na TAIFA RIPOTA September 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAZEE wa Njuri Ncheke wamemuonyesha mgongo Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kumuunga mkono  Waziri wa Usalama Kithure Kindiki kama kiongozi wao wa eneo la Mlima Kenya. 

Huku siasa za ubabe zikiendelea kushika kasi, Naibu Rais Rigathi Gachagua amepata pigo baada ya zaidi ya wazee takriban 2000 kumuidhinisha Waziri wa Usalama kuwa msemaji wa eneo hilo.

Kulingana na wazee hao kutoka Kaunti za Meru na Tharaka Nithi ,Waziri kindiki ndiye anayetosha kuwawakilisha kwa sababu ya uhusiano wake mwema na Rais William Ruto. Wanaamini Prof Kindiki ndiye njia yao nyoofu ya kumfikia Rais ili kuchochea maendeleo ya eneo la Mlima Kenya.

“Kwa ajili ya kuzingatia maendeleo, tunamuidhinisha Profesa Kithure Kindiki kuwa njia kati ya Rais na utawala wake. Tunaamini mamlaka yake ya kitaifa itasaidia kukuza uhusiano mwema na maeneo mengine,” alisema Adriano Aruyaru, Mwenyekiti wa Njuri Ncheke.

Hatua hii ni kinyume na matarajio ya Naibu Rais Rigathi Gachagua, kuwa mbabe wa eneo la mlima kenya, ikilinganishwa kwamba, Bw Gachagua amekuwa mstari wa mbele kuleta umoja wa eneo la hilo hasa katika wadhifa wake wa Naibu Rais.

Uamuzi huu unajiri takriban wiki mbili tu baada ya wabunge 69, kumchagua Prof  Kindiki kama msemaji na kiongozi wao wa eneo la Kati.

Naibu Rais hata hivyo alitangaza kujitenga na siasa za mlima Kenya Jumapili 15, Septemba 2024, alipowaonya viongozi wa mlima kujiepusha na siasa za ukabila na badala yake waangazie majukumu yao ya kuleta maendeleo katika maeneo yao husika.