Spika Kingi akataza maseneta kusafiri wasikosekane hoja ya kutimua Gachagua ikiwasili
SPIKA wa Bunge la Seneti Amason Kingi amepiga marufuku maseneta kusafiri nje ya nchi kabla ya hoja muhimu ya kumuondoa madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua kushughulikiwa.
Katika mawasiliano mafupi kwa maseneta, Spika Kingi alisema hakuna seneta au mfanyikazi wa Seneti anayefaa kuondoka nchini hadi washughulikie suala muhimu linalosubiriwa.
Gavana huyo wa zamani wa Kilifi pia aliagiza kwamba hakuna mikutano ya kamati au shughuli zozote zinazopaswa kufanywa nje ya Nairobi kati ya Jumanne Oktoba 8, 2024 na Jumamosi, Oktoba 19, 2024.
“Kama mnavyojua, Seneti ina shughuli kubwa inayokuja ya kuzingatiwa siku zijazo. Kwa kuzingatia uzito wa suala hili, ni muhimu tudumishe uwepo na umakini katika Seneti,” akasema Bw Kingi kwenye ilani ya ndani aliyotumia maseneta Oktoba 8, 2024.
“Ili kuafikia hili, safari zote za waheshimiwa maseneta na wafanyikazi wa Seneti nje ya nchi zimesitishwa mara moja,” akaongeza.
Bw Kingi alisema maagizo hayo yanalenga kuhakikisha kuwa maseneta wote wanashiriki katika shughuli hiyo muhimu bila usumbufu wowote.