Habari za Kitaifa

Tahadhari yatolewa trela lililobeba sumu kali ya Sodium Cyanide likianguka Kiambu

Na FATUMA BARIKI July 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WIZARA ya Afya imetoa tahadhari baada ya trela lililobeba sumu kali aina ya Sodium Cyanide kuanguka katika eneo la Kambembe, Rironi, Kaunti ya Kiambu.

Taarifa kutoka kwa Katibu wa wizara hiyo Mary Muthoni inasema kwamba umma unatahadharishwa dhidi ya kusogelea eneo hilo la mkasa, kwa sababu kemikali hiyo ni hatari mno kiasi cha kusababisha kifo iwapo mhusika anatagusana nayo kwa wingi.

Sodium Cyanide inatajwa kuwa mojawapo ya sumu kali zaidi duniani, kutokana na uwezo wake wa kusababisha kifo mara moja. Ina rangi nyeupe, na huweza kuchanganyika kwa wepesi na maji na vyuma pia, jambo linaloifanya kuwa hatari.

Ni madini ambayo yanatumika katika uchimbaji dhahabu, kutokana na uwezo wake wa kuyeyusha dhahabu kwa umakinifu mkubwa, kutoka kwa tope au mchanganyiko mwingine, katika shughuli inayofahamika kisayansi kama Cyanidation.