Habari za Kitaifa

TSC yaagizwa kupatia kipaumbele walimu wenye umri mkubwa wakati wa uajiri

Na LYNET IGADWAH May 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUME ya Huduma kwa Walimu (TSC) imeagizwa kuwasilisha takwimu za walimu wote waliosajiliwa na walio na umri wa zaidi ya miaka 40, katika hatua ya kushughulikia malalamishi ya muda mrefu kuhusu upendeleo katika mchakato wa uajiri wa walimu.

Hatua hii inafuatia wasiwasi kutoka kwa Wabunge kwamba TSC imekuwa ikiwapuuza walimu wengi wenye uzoefu na sifa kwa sababu tu wana umri wa zaidi ya miaka 45.

Uamuzi wa mwaka 2019 wa Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ulipata kwamba kigezo cha umri kilichowekwa na TSC kilikuwa cha ubaguzi na kilikiuka haki ya fursa sawa kwa wote.

“Tupeni takwimu za walimu waliosajiliwa na TSC wenye vyeti vya usajili na walio na zaidi ya miaka 40 ili tuweze kupima na kuangalia rasilmali zinazohitajika kuwaajiri,” alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Julius Melly, kwa maafisa wakuu wa TSC wakati wa kikao cha kujadili Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/26.

Timu ya TSC iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Fedha Cheptumo Ayabei ilieleza kuwa kigezo cha umri kinapewa uzito wakati wa mchakato wa uajiri, lakini wabunge hawakuridhishwa.

“Umri unapewa kipaumbele kulingana na miongozo ya ajira ambapo mtu ambaye amesubiri kwa muda mrefu na kuzeeka huongezewa alama 30 zaidi,” alisema Bw Ayabei.

Hata hivyo, kamati ilisisitiza kuwa mwalimu yeyote anaweza kuajiriwa hadi na ikiwa ni miaka miwili kabla ya kustaafu kwa sababu si kosa lake kutoajiriwa akiwa na zaidi ya miaka 45.

Kabla ya kuajiri walimu wakongwe, wabunge walisisitiza kuwa walimu hao lazima wapendekezwe na shule ambazo wamekuwa wakifundisha ili kuhakikisha haki katika mchakato wa uajiri.

Mwaka jana, serikali iliwabadili walimu 39,550 wa shule za sekondari msingi kutoka mikataba ya muda hadi ajira ya kudumu, huku walimu wengine 8,378 wa shule za msingi wakihamishwa kufundisha katika shule za sekondari msingi.

Lakini licha ya juhudi hizi, uhaba mkubwa wa walimu bado upo katika shule 20,000 za sekondari msingi ambapo data ya TSC inaonyesha upungufu wa walimu 72,422.

Upungufu wa wafanyakazi shuleni umesababisha walimu kulemewa na kazi, msongamano wa wanafunzi madarasani na ukosefu wa walimu maalumu wa masomo wanaohitajika kutekeleza mtaala wa CBC ipasavyo.

“Tumezungumza na Hazina ya Taifa na huenda kwa sababu ya hali ya kifedha, inaonekana tutapewa pesa za kuajiri walimu wa muda na siyo kuwaajiri wa kudumu,” alisema Bw Cheptumo.

Kwa mwaka wa fedha unaoanza Julai, Hazina ya Taifa haijatenga fedha kuajiri walimu wa muda kuwa wa kudumu, jambo linalotatiza ajira ya walimu wa zaidi ya miaka 45.

TSC imetengewa Sh387.7 bilioni kwa mwaka unaoanza Julai, lakini maeneo muhimu kadhaa hayajatengewa fedha za kutosha, yakiwemo matibabu ya walimu, na Mkataba wa Maelewano (CBA) wa 2025–2029.

CBA ya sasa inatarajiwa kuisha mwishoni mwa Juni ili kutoa nafasi kwa mazungumzo ya mkataba mpya, ambapo Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari (KUPPET) kimeashiria kupendekeza nyongeza ya marupurupu ya mazingira magumu.

Hii inajiri wakati serikali inapanga kutekeleza ripoti ya mwaka 2019 inayolenga kurekebisha maeneo yanayotambuliwa kuwa ya mazingira magumu ili kuokoa Sh6 bilioni kila mwaka kwa kupunguza malipo kutoka Sh25 bilioni hadi Sh19 bilioni.