Habari za Kitaifa

Uhaba wa mahindi: Serikali kuruhusu mahindi ya njano kuagizwa nchini bila ushuru kupunguza bei ya unga

Na LINET OWOKO NA BARNABAS BII April 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WIZARA ya Kilimo inapanga kuruhusu uagizaji wa magunia 5.5 milioni ya mahindi ya njano ili kupunguza shinikizo kwa mahindi meupe yanayokuzwa nchini, ambayo bei yake imepanda kwa hadi asilimia 26.47 tangu Desemba 2024.

Waziri wa Kilimo, Mutahi Kagwe, alisema kuwa serikali itatoa msamaha wa ushuru wa asilimia 50 kwa mahindi ya njano kwa mwaka mmoja.

“Wizara ya Kilimo na Ustawishaji ya Mifugo inatambua ushindani unaoongezeka kati ya wazalishaji wa chakula cha mifugo na wasagaji wa unga wa mahindi kwa matumizi ya binadamu kutokana na upungufu wa mahindi nchini. Kutokana na ongezeko hili la mahitaji, bei ya gunia la kilo 90 imeongezeka kwa karibu asilimia 26 ikilinganishwa na miezi mitatu iliyopita,” alisema Waziri Kagwe.

Kupanda kwa bei ya mahindi kumefanya gharama ya unga wa mahindi kupanda, kwani wasagaji wanapandisha bei.

Data kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu Kenya (KNBS) zinaonyesha kuwa pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi iliuzwa kwa wastani wa Sh165.05 mnamo Machi—ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kwa miezi 13.

Bei hiyo inaashiria ongezeko la asilimia 2.94 kutoka Februari na asilimia 14.11 tangu Oktoba mwaka jana, 2024.

Wasagaji wa unga wanasema kupanda kwa bei kunatokana na upungufu wa mahindi nchini, hali inayopelekea kutegemea uagizaji kutoka Tanzania.

“Kilimo cha mahindi kinapungua, na wafanyabiashara wanashikilia akiba yao wakitarajia ongezeko la bei,” alisema Paloma Fernandes, Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Wasagaji Nafaka.

“Wazalishaji wa chakula cha mifugo wanawania mahindi yale yale, kwani hakuna msamaha wa ushuru ulioidhinishwa kwa mahindi yanayoagizwa kwa chakula cha mifugo, hali inayoongeza mahitaji zaidi,” aliongeza.

Waziri Kagwe alisema kuwa serikali itaruhusu wazalishaji wa chakula cha mifugo wenye uwezo wa kutosha kuagiza mahindi ya manjano ili kupunguza shinikizo kwa mahindi meupe ya ndani.

“Lengo ni kupunguza kutegemea mahindi meupe kwa kuwashawishi wazalishaji wa chakula cha mifugo kutumia mahindi ya njano. Hii itawawezesha wasagaji wa unga wa mahindi kwa matumizi ya binadamu kupata mahindi kwa bei nafuu, hivyo kupunguza gharama ya uzalishaji na kusaidia kupunguza bei ya unga kwa watumiaji,” alisema Bw Kagwe.