Habari za Kitaifa

Uhuru atakiwa akohoe ajibu ‘mashtaka’ ya Raila

Na MWANGI MUIRURI August 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

BAADHI ya wandani wa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua katika ukanda wa Mlima Kenya sasa wanataka Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta aseme wazi ikiwa alitoa kibali kwa wandani wa Bw Raila Odinga kujiunga na serikali ya Rais William Ruto.

Haya yanajiri majuma mawili baada ya Bw Gachagua kutangaza waziwazi kwamba yeye na Bw Kenyatta wanashirikiana kisiasa kwa lengo la kupalilia umoja wa eneo hilo na kupanga mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

“Baada ya mimi kuomba msamaha kwa familia ya Kenyatta, Uhuru alinipigia simu akakubali hatua hiyo. Mama yake alinisamehe na kuna miradi mingi tunayotekeleza pamoja,” Bw Gachagua alitangaza Agosti 4 wakati wa mahojiano na vituo vya habari vya lugha za Mlima Kenya.

Wandani wa Naibu Rais waliozungumza na Taifa Leo walisema wanashuku ufichuzi wa Bw Odinga kwamba Bw Kenyatta alimshauri ashirikiane na Dkt Ruto.

“Huu ni ujanja wa kisiasa ambao haufai kuaminiwa haraka hadi pale utakapothibitishwa na Rais Mstaafu mwenyewe,” akasema Seneta wa Kiambu Karungo wa Thang’wa.

Kulingana na gavana wa zamani wa Kiambu, Ferdinand Waititu, kauli ya Bw Odinga ililenga kumnyima Bw Gachagua ushawishi wa Mlima Kenya na kusawiri eneo hilo kama ambalo lingali limegawanyika kisiasa.

“Wakazi wa Mlima Kenya wanastahili kuendelea kuwa waangalifu zaidi kuhusiana na karata za kisiasa ambazo Rais Ruto na Bw Odinga wanacheza katika eneo hili kwa kutaja jina la Rais Mstaafu,” akasema.

Bw Waititu alisema lengo la Bw Odinga ni kuonyesha kuwa roho ya Bw Kenyatta bado iko katika muungano wa Azimio la Umoja na hivyo wakazi wa Mlima Kenya hawafai kuunga mkono juhudi za kuunganisha eneo la Mlima Kenya kisiasa.

“Ni kweli wapiga-kura wetu wamevunjika moyo kwani walipiga kura ili wavune matunda ya kuwa serikaliNni na Bw Odinga akae katika upinzani. Wamekasirika kwamba Rais alimleta Odinga serikalini bila kutushauri sisi kama viongozi wao,” akasema Mbunge wa Naivasha, Jayne Kihara, mshirika wa Bw Gachagua.

Bi Kihara akasema, “watu hawaamini serikali hii inayotajwa kama jumuishi kwani wanaichukulia kama ya kusaliti Gachagua kuelekea 2027. Hii imemwongezea umaarufu Bw Gachagua.”

Mbunge huyo wa Naivasha anasema kuna dalili kwamba njama za kumhujumu Bw Gachagua katika Mlima Kenya bado zinaendelea.

“Inaonekana kuwa Bw Odinga analenga kushawishi Bw Kenyatta asiungane na Bw Gachagua kwa sababu rais wao wa zamani angali katika Azimio,” Bi Kihara anaongeza.

Gavana wa Nyeri, Bw Mutahi Kahiga anaamini kuwa Bw Odinga anajificha serikalini tu kwa muda kabla ya kuivuruga na kuondoka.

“Tusubiri tuone, imekuwa tabia yake kuingia serikalini na kisha kuondoka baada ya kuruvuga mambo. Wakati huu, tunamuunga mkono ili kupata utulivu serikalini ili tutoe huduma kwa wananchi. Lakini hivi karibuni tutaanza kuruka huku na kule kuokoa serikali yetu,” akasema.

Kwa upande wake Mbunge Maalum Teresiah Wairimu anasema kuwa baada ya jaribio la kumwondoa mamlakani Bw Gachagua kuonekana kuwa gumu, waliopanga njama hizo sasa wanaendesha mpango wa kumhujumu, hali inayomjengea sifa.

“Naibu Rais sasa anahusudiwa zaidi katika eneo la Mlima Kenya. Lakini anapigwa vita kupitia kurejeshwa kwa pombe haramu, kucheleweshwa kwa malipo kwa wakulima wa kahawa na majani chai na kupigwa vita kwa mfumo wa ugavi wa mapato wa ‘mtu mmoja, kura moja, shilingi moja” Bw Wairimu akasema.

Mbinu nyingine zinazoendelezwa kumpiga vita Bw Gachagua ni kupuuzwa kwa ‘injili’ yake ya umoja wa Mlima Kenya kama uendelezaji wa ukabila, kuwaonya viongozi waliochaguliwa wasihudhurie mikutano yake na kukuza dhana kuwa Bw Gachagua anaendeleza masilahi yake binafsi serikalini.

Akiongea katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet mnamo Jumatano, Bw Odinga alisema vijana wa Gen-Z walipoanza maandamano Juni 18 hadi wakavamia Bunge Juni 25, 2024, “Bw Kenyatta alinipigia simu na kunishauri nizungumze na Rais Ruto kuhusu namna ya kuokoa nchi hii.”

“Sasa tunamtaka Bw Uhuru kujitokeza wazi na kusema iwapo ni kweli kuwa moyo wake ungali katika Azimio. Aseme ikiwa anataka Mlima Kenya iunge mkono Azimio au iegemee umoja unaoendelezwa na Bw Gachagua,” Bw Waititu akasema.

Naye Mbunge wa zamani wa Gatanga Nduati Ngugi alisema: “Tumekuwa tukihudhuria mikutano mingi ya ushauriano katika siku za hivi karibuni lakini hatujawahi kuambiwa kuwa Bw Kenyatta anataka tushirikiane na Bw Odinga kuokoa Rais Ruto.”

Mbunge huyo wa zamani alidai kuwa Bw Kenyatta huzungumza nao kupitia Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni lakini kufikia sasa hawajajulishwa kuhusu madai mapya yaliyotolewa na Bw Odinga juzi.

Bw Ngugi anasema kuna dalili kuwa Bw Odinga hasemi ukweli kwa sababu wandani wote wa Bw Kenyatta wamekuwa wakipinga hatua ya Rais Ruto kujumuisha viongozi wa upinzani katika baraza lake la mawaziri.