Habari za Kitaifa

Ukweli wa mambo: Ruto hakumtambulisha Soipan Tuya kama Ex wake

Na MIKE YAMBO, BENSON MATHEKA August 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KUNA video inayosambazwa mtandaoni ikinuiwa kumuonyesha Rais wa Kenya William Ruto akimtambulisha Waziri Mteule wa Ulinzi Soipan Tuya, kama mpenzi wake wa zamani.

Video hii, ambayo imesambazwa haswa kwenye X, YouTube, na hata TikTok – imevutia umakini mkubwa na kuzua mdahalo, huku watazamaji wengi wakiamini kuwa ni ya kweli.

Muktadha

Mnamo Julai 11, 2024, Rais William Ruto alivunja  baraza lake la mawaziri kufuatia wiki kadhaa za maandamano nchini kote kupinga mapendekezo ya nyongeza ya ushuru. Uamuzi huu ulijiri baada ya ghasia zilizomfanya  kutotia saini Sheria ya Fedha ya 2024.

Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni, Ruto alitangaza kuwa angeshauriana  kwa kina ili kuunda serikali  jumuishi, kwa kujumuisha vyama  na sekta mbalimbali. Licha ya juhudi hizi, uteuzi wake wa  baraza jipya la mawaziri umekosolewa vikali. Wakosoaji wanahoji kuwa baadhi ya mawaziri walioteuliwa upya, kama vile Kithure Kindiki ( Usalama wa Ndani) Aden Duale(Mazingira), na Soipan Tuya( Ulinzi), hawawakilishi mabadiliko yanayohitajika kushughulikia changamoto za nchi.

Uchambuzi wa Video

Utathmini wa video husika unaonyesha ilinaswa Siku ya Kitaifa ya Kupanda Miti Mei 10, 2024, ambapo Rais Ruto alikuwa akiongoza zoezi  hili  katika Msitu wa Kiambicho Kaunti ya Murang’a kama inavyoonekana kwenye video iliyochapishwa kwenye YouTube ya Ikulu ya Kenya.  Tukio hili pia liliangaziwa na NTV. Katika picha ya awali, Ruto anazungumza kwa ufupi kuhusu uhusiano wake na mkewe, Rachel Ruto kabla ya kumtambulisha Waziri Soipan Tuya. Hata hivyo, video hiyo iliyobadilishwa imehaririwa ili kuingiza taarifa ya uongo kuhusu Soipan Tuya, na hivyo kuibua hisia kwamba Ruto alifichua kibinafsi kuhusu uhusiano wao wa awali.

Tofauti za Video na Sauti

– Masuala ya Kusawazisha Midomo: Uchunguzi wa karibu wa video unaonyesha kwamba usawazishaji kati ya midomo ya Ruto na sauti haiendani, ishara ya kawaida ya kuvurugwa kwa video.

– Ubora wa Sauti: Klipu ya sauti inayomtaja Soipan Tuya kama mpenzi wa zamani wa Ruto ina sauti isiyolingana ikilinganishwa na hotuba nyingine, ikionyesha kuwa ilikatwa kutoka kwa video asili.

Uamuzi

Video inayodai kuwa Rais William Ruto alimtambulisha Soipan Tuya kama mpenzi wake wa zamani ni feki iliyobuniwa kueneza simulizi potofu.