Habari za Kitaifa

Upinzani wataka Trump achunguze polisi wa Kenya walivyoidhinishwa kutumwa Haiti

Na EVANS JAOLA November 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BAADHI ya viongozi wa upinzani sasa wanataka uchunguzi ufanywe kuhusu jinsi kibali kilitolewa kwa Polisi wa Kenya kupelekwa Haiti.

Viongozi hao wakiongozwa na kiongozi wa chama cha Democratic Action Party DAP-K Eugene Wamalwa wametaka uchunguzi ufanywe iwapo kilichochochea polisi hao kutumwa ni pesa ambazo utawala wa Rais William Ruto ulipata ili ukubali mpango huo.

Bw Wamalwa amemtaka Rais mteule wa Amerika, Donald Trump kuchunguza upya makubaliano kati ya Kenya na Amerika yaliyonuia kusaidia kukabiliana na ongezeko la uhalifu nchini Haiti.

Bw Wamalwa aliitaka serikali ya Amerika kukagua fedha zinazotengewa mpango huo, kuhakikisha kila senti inatumika ipasavyo kushughulikia usalama wa Kenya.

Mnamo Alhamisi, Rais Ruto alizungumza na Waziri wa Masuala ya Nje wa Amerika, Antony Blinken kupitia simu kujadili hatima ya kikosi cha polisi nchini Haiti.

IMETAFSIRIWA NA WINNIE ONYANDO