Uteuzi wa Ruku wamnyoshea Rais njia kabla ya ziara ya Mlima Kenya
UTEUZI wa Mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku kama waziri unatarajiwa kuchemsha siasa za Mlima Kenya, zikiwa zimesalia siku za kuhesabu tu kabla ya Rais William Ruto kutembelea eneo hilo.
Bw Ruku aliteuliwa kama waziri wa utumishi wa umma na iwapo ataidhinishwa na bunge, atachukua wadhifa huo kutoka kwa Justin Muturi ambaye alifutwa na Rais William Ruto mnamo Jumatano.
Mbunge huyo anatoka eneo moja na Bw Muturi ambaye aliwakilisha eneo hilo kati ya 2002-2007 kupitia chama cha Kanu, wakati huo likifahamika kama Siakago.
Wakati ambapo taarifa zilitoka kuhusu kuteuliwa kwake, Bw Ruku alikuwa na Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, akikagua mradi wa kunyunyizia mashamba maji wa Kanyuambora katika eneobunge lake.
Mradi huo umeigharimu serikali Sh258 milioni na unatarajiwa kuinua kilimo na mapato ya wakulima kutoka eneo hilo.
Bw Ruku, 45 anahudumu muhula wake wa kwanza bungeni na alichaguliwa kupitia DP mnamo 2022. Alilemewa ubunge 2013 na Muriuki Njagagua kabla ya kupoteza useneta 2017 kwa waziri wa zamani Njeru Ndwiga.
Uteuzi wake umekuja wakati ambapo Bw Muturi amekuwa akifarakana na Rais Ruto huku akilaumu serikali kwa kutoweka juhudi za kutosha kukabiliana na visa vya utekaji nyara na watu kupotea kisha kupatikana wamekufa.
Mnamo Jumanne, Rais alionekana kuchoshwa na ukosoaji wa Bw Muturi aliposema alilemewa na kazi alipohudumu kama mwanasheria mkuu.

“Nilikuwa na tatizo na mwanasheria mkuu wa wakati huo. Alikuwa hawajibikii vyema majukumu yake lakini sasa nina mwanamke mchapa kazi na nawahakikishia suala la kuanzishwa kwa ‘Hazina ya Fedha ya Waislamu’ litatuliwa miezi michache inayokuja,” akasema Rais. Alikuwa akiongea ikulu alipowaalika Waislamu kushiriki iftar naye Jumanne usiku.
Bw Muturi Jumatano alikanusha hilo na kusema hakukuwa na mwanya wa kisheria wa kuanzishwa kwa hazina hiyo akimlaumu kiongozi wa nchi kwa kumwinda kisiasa.
Uwaziri wa Bw Ruku unatarajiwa kuchemsha siasa za mlimani hasa Embu huku wadadisi wa kisiasa wakifasiri kuwa wizara hiyo kusalia kaunti hiyo ililenga kupunguza uhasama na hasira ambazo zingeongezeka dhidi ya Ruto.
“Wizara imesalia Embu na hilo litampa Rais nafasi ya kueleza eneo hilo kwenye ziara yake kuwa bado anawajali wala si maadui wake. Anatuma ujumbe kuwa ana tashwishi na mwanasiasa (Muturi) na si wananchi wa kawaida ndiposa amerudisha kiti eneo hilo,” akasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo.
“Sasa hatakuwa na tatizo kutembea Embu kwa sababu mawaziri, makatibu na maafisa wa serikali watanyoosha mambo kimapokezi. Hata kama hawatamchagua 2027 kwa asilimia 100, mapokezi yatakuwa mazuri Embu,” akaongeza.
Rais alizuru Embu miezi minne iliyopita ambapo alizomewa kwenye hafla ya kutawazwa kwa Askofu Peter Kimani kama askofu wa kanisa la Kianglikana Dayosisi ya Embu.