Habari za Kitaifa

Vijana waandamana kupinga Nyachae, wazee kuhojiwa kwa uenyekiti wa IEBC

Na WINNIE ONYANDO March 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

VIJANA Jumatatu waliandamana nje ya jengo ambalo mahojiano ya kumteua mwenyekiti mpya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) yalikuwa yakiendelea huku wakidai kuwa baadhi ya walioteuliwa walikuwa wazee.

Mwenyekiti wa Shirika la Kenya Youth Johnmark Ababu aliongoza maandamano hayo akidai kuwa wadhifa kama huo unahitaji vijana.

Mahojiano hayo yanaendelea ili kumpata mrithi wa aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati aliyeaga dunia mwezi jana.

Kulingana naye, baadhi ya vijana walituma ombi lao ila hakuna hata moja aliyebahatika kuorodheshwa kwa mahojiano hayo.

“Baadhi ya watu ambao majina yao yaliorodhoshwa ni wazee. Tunataka vijana pia na hakuna hata kijana mmoja katika orodha hiyo,” akasema Bw Ababu.

Kando na hayo, shirika hilo linampinga  Charles Nyachae ambaye pia ni miongoni mwa waliorodheshwa kwa mahojiano hayo. Bw Nyachae ni mmoja wa watu ambao walifanyiwa mahojiano siku ya Jumatatu

Shirika hilo linadai kuwa Bw Nyachae hafai kushikilia wadhifa huo kutokana na masuala mbalimbali ya kimaadili.

“Pingamizi hilo liliwasilishwa katika risala ya Machi, 17, 2025, iliyoelekezwa kwa mwenyekiti wa jopo la uteuzi wa IEBC. Pingamizi hilo linazua wasiwasi mkubwa kuhusu kufaa kwa Nyachae kwa jukumu hili muhimu, na kusisitiza umuhimu wa uadilifu na viwango vya maadili katika mchakato wa uchaguzi nchini Kenya,” akasema Bw Ababu.

Naye Mourice Masiga, katibu wa shirika hilo anasema kuwa vijana wanafaa kupewa nafasi kama hizo kwani wana uwezo na tajriba hitajika.

“Kwani sisi kama vijana tutatambulika lini. Hata sisi tuna uwezo wa kushikilia wadhifa kama hizo,” akasema Bw Masiga.

Aliyekuwa msajili wa Idara ya Mahakama Anne Amadi, Charles Nyachae na Mwenyekiti wa Bodi ya Kawi Joy Brenda Mdivo ni miongoni mwa wagombeaji 11 walioteuliwa kuwania nafasi ya uenyekiti wa IEBC.