Habari za Kitaifa

Wafuasi wa Ruto, Gachagua wapigana hata kabla ya Rais kuanza ziara Mlimani

Na MARTIN MWAURA March 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAFUASI wa Rais William Ruto na wale wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua Jumapili walipigana katika eneobunge la Gatanga, Kaunti ya Murangá kuelekea ziara ya Rais inayoanza Jumanne Mlima Kenya.

Makundi hayo mawili yalipambana katika Kanisa la AIPCA Mwagu Gatanga baada ya gari lililomilikiwa na Diwani wa Kariara Gichobe Mbatia kuharibiwa na makundi ya vijana. Tukio hilo lilijiri wakati ambapo ibada ilikuwa ikiendelea.

Baada ya ibada, diwani huyo pamoja na Seneta wa Murangá Joe Nyutu na Mbunge wa Gatanga Edward Muriu ambao ni wandani wa Bw Gachagua, walimshutumu Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Murangá Betty Maina kwa kuwadhamini wahuni hao.

Bw Mbatia alisema wahuni hao ambao walijihami kwa panga na silaha butu walisafirishwa kutoka Nairobi.

“Walisafirishwa kwenye gari aina ya pickup iliyokuwa ikiendeshwa na mwanaume anayefanyia kazi Bi Maina. Wafuasi wetu waliwanyaka wahuni watatu na wakawapa polisi  lakini wakaachiliwa kutokana na shinikizo kutoka juu,” diwani huyo akasema.

Hata hivyo, Bi Maina alikanusha madai hayo akisema tukio hilo ni ubabe wa kisiasa kuelekea kura ya 2027. Aliweka wazi kuwa alialikwa kanisani humo na askofu na alishangazwa kusikia kulikuwa na mtafaruku nje wakati maombi yalikuwa yakiendelea.

“Mwanzo nilifikiria kuwa tulikuwa tumevamiwa na ni baada ya ibada ndipo nikafahamu kilichotokea. Makabiliano yalikuwa kati ya wafuasi wa Muriu na diwani kuhusu siasa za 2027,” akasema.

Mwakilishi huyo alisema uhasama kati ya mirengo inayounga Bw Gachagua na Rais Ruto ulianza Jumamosi kwenye hafla ya harusi ya kitamaduni Gatanga.

“Niliwaomba Nyutu, Muriu na diwani huyo wasizungumzie siasa ili wasivuruge hafla hiyo. Hata hivyo, walijibu kwa kupiga kelele wakisema ‘Ruto Lazima Aende’  na pia wakanizomea na wafuasi wangu,” akasema Bi Maina.

Seneta Nyutu alisema kuwa  ni aibu kuwa wale ambao wanaunga mkono serikali walikuwa wakitumia polisi na wahuni kuwanyanyasa wapinzani wao.

“Bi Maina sasa anatumia urafiki wake na serikali kuwatishia watu wakiwatumia wahuni ambao wanalindwa na polisi,” seneta huyo akasema.

Aliongeza kuwa rais yupo huru kutembelea eneo hilo ila asije kuhubiri uongo na badala yake aseme miradi ya maendeleo ambayo ameitekeleza.

Wakati wa ghasia hizo msaidizi wa Bw Muriu alijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ya Kirwara.

“Hatujawahi kushuhudia ghasia Gatanga na leo tumewaona watu ambao walimwondoa Gachagua mamlakani wanamuunga mkono Rais Ruto wakizua ghasia kanisani,” akasema Bw Muriu.

Kamanda wa Polisi wa Murangá Benjamin Kimwele alikanusha madai kuwa polisi walikuwa wamewanyaka wahuni waliodaiwa kusafirishwa na kuwawaachilia.

“Hakukuwa na ushahidi wowote kuwa watu watatu waliozuiliwa na kuwaachiliwa na polisi ndio waliharibu gari. Walitajwa na wakazi kwa sababu walikuwa wageni eneo hilo na walikuwa wameandamana na viongozi wanawake,” akasema Bw Kimwele.

“Kwa sababu hakukuwa na ushahidi, polisi hawangewazuilia. Walizuiliwa kuwatorosha kutokana na ghadhabu za umma waliotaka kuwapiga,” akaongeza.

imetafsiriwa na Cecil Odongo