Watoto wengi kufariki baada ya Amerika kuondoa msaada –UN
UMOJA wa Mataifa (UN) umeonya kuwa kuondolewa kwa msaada na Amerika kunaweza kuchangia ongezeko la vifo vya watoto katika mataifa ambayo hutegemea misaada ya kibinadamu.
Hatua hiyo, kulingana na shirika hilo, itarudisha nyuma hatua ambazo zimepigwa kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, ambayo imekuwa ikipungua tangu 2015.
Kuondolewa kwa misaada kwa mataifa hayo kumechangia kupungua kwa idadi ya wahudumu wa afya, kufungwa kwa vituo vya afya, kuvurugwa kwa mipango ya utoaji chanjo na ukosefu wa dawa na vifaa vya kutibu magonjwa kama malaria.
“Kuondolewa kwa ufadhili pia kutaathiri uwezo wa nchi husika kutekeleza mipango ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu,” inasema UN.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, alishauri kwamba kufuatia hatua ya Amerika kuondoa ufadhili, jamii za ulimwenguni zinapaswa kushirikiana “kulinda afya ya watoto.”
Dkt Tedro alisema kuwa karibu nusu ya idadi ya vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano hutokea ndani ya mwezi wa kwanza baada ya kuzaliwa kwao.
“Mbali na vifo vinavyotokea kutokana na hitilafu zinazotokea akina mama wanapojifungua, magonjwa ya kuambukizwa, malaria na nimonia na ugonjwa wa kuendesha pia husababisha vifo vya watoto,” akaeleza.
Vilevile, asilimia 45 ya watoto wanazaliwa kabla ya muda kutimu wakati wa kuzaliwa kutokana na maradhi ya yanayowakumba akina mama wajawazito.
Dkt Tedro aliongeza kuwa ni muhimu kwa nchi za ulimwenguni kukabiliana na maradhi hatari kama malaria.Aidha, kulingana na ripoti hiyo ya UN-IGME watoto katika mataifa yaliyoko kusini mwa bara la Afrika ndio wako katika hatari kubwa ya kufa kabla ya kutimu umri wa miaka mitano.
Data inayolenga Kenya inaonyesha kuwa watoto 41 kati ya 1,000 hupoteza maisha yao kabla ya kutimu umri wa miaka mitano.Katika mwaka wa 2021 Kenya iliandikisha visa 27, 720 vya watoto kuzaliwa kabla ya muda wao kutimu.
Mnamo 2023, jumla ya watoto 32, 000 walikufa nchini Kenya kabla ya kufika umri wa miaka mitano.
“Idadi tofauti ya watoto wanaokufa katika nchi mbalimbali inasalia kuwa changamoto kubwa ya nyakati hizi. Kupunguza utofauti huo ni jambo la lazima na hatua muhimu katika kufikia maendeleo endelevu na usawa ulimwenguni. Kila mtoto anahitaji nafasi ya kuishi, na ni wajibu wetu wa pamoja kuhakikisha kuwa hamna mtoto anayeachwa nyuma,” akasema Li Junhua ambaye ni msaidizi wa Katibu Mkuu wa UN anayesimamia Masuala ya Kiuchumi na Kijamii.
Wanachama wa shirika hilo sasa wanatoa wito kwa serikali za nchi mbalimbali, wafadhili na washirika katika sekta za umma na kibinafsi kuongezea juhudi za kuwezesha akina mama wajawazito kupata huduma za afya na lishe bora kwa watoto wao wachanga.