Habari za Kitaifa

Wetangu’la aita wabunge kuamua uteuzi wa wandani wa Uhuru kuwa mawaziri

Na CHARLES WASONGA January 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BUNGE la Kitaifa  litaamua wiki ijayo iwapo wandani wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Mutahi Kagwe, Lee Kinyanjui na William Kabogo, watahudumu kama mawaziri au la.

Hii ni baada ya Spika Bunge hilo Moses Wetang’ula kuitisha vikao viwili maalum Alhamisi kujadili na kupigia kura ripoti ya Kamati ya Uteuzi itakayowapiga msasa Jumanne.

“Baada ya kupokea ombi mnamo Januari 3, 2025, nimekubali na kutenga Alhamisi, Januari 16, 2025 kama siku ya Vikao Maalum vya Bunge la Kitaifa. Vikao hivyo vitafanyika katika ukumbi wa mijadala wa Bunge la Kitaifa, majengo ya Bunge, Nairobi, kuanzia saa nne asubuhi na kuanzia saa nane na nusu alasiri (kwa kikao cha asubuhi na alasiri, mtawalia),” Bw Wetang’ula akasema kwenye tangazo lililochapishwa magazetini jana.

“Katika vikao hivyo, wabunge watajadili na kupigia kura ripoti ya Kamati ya Uteuzi kuhusu shughuli ya kuwapiga msasa mawaziri wateule, ripoti kuhusu Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Mahusiano ya Kitaifa kuhusu watu waliopendekezwa kuwa mabalozi na ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Leba kwa watu walioteuliwa kuhudumu kama naibu mwenyekiti na wanachama wa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), miongoni mwa masuala mengine yenye umuhimu wa kitaifa,” Bw Wetang’ula akaongeza.

Katika mabadiliko serikalini ambayo Rais William Ruto alitangaza mnamo Desemba 19, 2024, alimpendekeza Bw Kagwe, kuwa Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo.

Bw Kagwe ni Seneta wa zamani wa Nyeri na Waziri wa Afya wakati wa utawala uliopita wa Bw Kenyatta.

Naye Bw Kinyanjui ambaye ni Gavana wa zamani wa Nakuru alipendekezwa kuwa Waziri wa Biashara na Viwanda huku Bw Kabogo ambaye  alihudumu kama Gavana wa Kiambu kuanzia 2023 hadi 2027 akipendekezwa kuwa Waziri wa ICT na Uchumi wa Kidijitali.

Uteuzi wa watatu hao ulijiri siku chache baada ya Rais Ruto kumtembelea Bw Kenyatta nyumbani kwake kijiji cha Ichaweri, Kiambu, katika kile kilichosawiriwa kuwa sehemu ya mpango wake wa kuokoa kudorora kwa ushawishi wake katika eneo la Mlima Kenya.

Hii ni baada ya wakazi wa eneo hilo, lililompigia kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa 2022, kumuasi kwa kuidhinisha kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mwaka jana.

Bw Kagwe anatajiwa kujaza nafasi ya aliyekuwa Waziri wa Kilimo Dkt Andrew Karaja ambaye sasa ameteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Brazil huku Bw Kabogo akichukuwa nafasi ya Dkt Margaret Nyambura ambaye amependekezwa kuwa balozi wa Kenya nchini Ghana.

Kwa upande wake Bw Kinyanjui anatarajiwa kuchukua nafasi ya Bw Salim Mvurya aliyehamishwa hadi Wizara ya Michezo kufuatia uhamisho wa Bw Kipchumba Murkomen hadi Wizara ya Usalama wa Ndani.