Habari za Kitaifa

Wizara ya Ulinzi yatahadharisha kuhusu tangazo feki la usajili wa makurutu KDF

Na CHARLES WASONGA August 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WIZARA ya Ulinzi imewataka wananchi kupuuzilia mbali tangazo kuhusu usajili wa makurutu wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) linalosambazwa mitandaoni, likidaiwa kutolewa kwa niaba ya jeshi hilo, ikisema tangazo hilo ni feki.

Kwenye taarifa iliyochapishwa katika gazeti la Daily Nation, toleo la Agosti 20, 2024, Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma katika Wizara hiyo Bi Grace Mwanja, amefafanua kuwa KDF haijaanza shughuli ya usajili wa makurutu na kwamba tangazo hilo,  “limedhaminiwa na matapeli.

“Wizara ingependa kujulisha umma kuwa KDF haijatoa tangazo lolote la usajili wa makurutu na haina mipango ya kuendesha usajili wowote wakati huu. Wizara inasisitiza kuwa shughuli rasmi ya usajili wa makurutu wa KDF itatangazwa kupitia majukwaa rasmi ya vyombo vya habari, tovuti ya wizara (www.mod.go.ke) na akaunti rasmi za mitandao ya kijamii za KDF,” akaeleza.