Habari za Kitaifa

Yafichuka Ruto alizindua miradi iliyoanzishwa na Uhuru ziarani Kisii

Na RUTH MBULA August 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

IMEBAINIKA kuwa baadhi ya miradi iliyozinduliwa na Rais William Ruto katika eneo la Gusii, ilianzishwa na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta.

Uchambuzi wa ziara ya Rais Ruto uliofanywa na Taifa Leo unafichua kuwa miradi mingi ambayo rais alizindua ilianzishwa kabla aingie uongozini na kwamba ilikuwa katika hatua za mwisho kukamilika.

Katika ziara yake, Rais Ruto aliidhinisha ujenzi wa hospitali ya kutibu saratani katika Mji wa Kisii na akadokeza kuwa mara tu kituo hicho kitakapokamilika, kitakuwa cha mabadiliko katika utoaji wa huduma muhimu kwa wagonjwa.

Katika hotuba yake, Dkt Ruto hakutoa dokezo lolote kwamba ufadhili huo ulipatikana kupitia mkopo kutoka Saudi Arabia na mtangulizi wake, Bw Kenyatta, kujenga vituo vinne vya aina hiyo nchini.

Bw Kenyatta alipozuru Kisii mwaka wa 2019, alisema, “Kuongezeka kwa visa vya saratani ni jambo linalotia wasiwasi sana. Utawala wangu umekusanya rasilimali kujenga vituo vinne vya kushughulikia ugonjwa huo nchini. Nina furaha kuripoti kwamba Kisii itanufaika na mpango huu.”

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu inaonyesha kuwa michakato yote ya mradi ilikuwa imekamilika, na kwamba Kenya ilipokea mkopo wa kujenga Kituo cha Saratani Kisii.

“Mradi huo utajengwa kupitia mkopo ambao mikataba yake ilitiwa saini Juni 3, 2015 kati ya Jamhuri ya Kenya (mkopaji) na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Uchumi Afrika (BADEA) kwa Sh1 bilioni katika soko la fedha lililokuwepo na Aprili 12, 2017 kati ya Mfuko wa Maendeleo wa Saudi (SFD) na Jamhuri ya Kenya kilikuwa Sh bilioni 1,” ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilisoma.

Naye Rais Ruto alipozungumza mjini Kisii wiki hii, alisema, “Kama mjuavyo, mradi huu umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu lakini nilitembelea Saudia mwaka jana na kukubaliana nao kutusaidia ili serikali yetu ijenge kituo bora cha saratani hapa Kisii.”

Katika eneo la Nyamira tena, Rais Ruto alizindua ukarabati wa barabara ya Eronge (D209).

Hata hivyo, barabara hiyo hiyo ilizinduliwa na aliyekuwa Waziri wa Barabara, James Macharia akishirikiana na mwenzake wa Wizara ya Mambo ya Ndani wakati huo Dkt Fred Matiang’i.

Dkt Ruto pia alizindua Barabara ya Sirare-Kisii-Ahero, ambayo ujenzi wake ulianza wakati wa utawala wa Bw Kenyatta