Hatuhitaji marubani tena – Trump
Na WAANDISHI WETU
RAIS wa Amerika Donald Trump, ametilia shaka uwezo wa marubani kuendesha ndege za kisasa.
Akizungumza siku mbili baada ya ndege ya Ethiopia kuanguka na kuua watu 157 wakiwemo Wakenya 32, rais huyo mbishi alisema ndege zimekuwa ngumu zaidi kuendesha, na hivyo zinahitaji wataalamu wa teknolojia za kisasa zaidi kuliko marubani.
“Marubani hawahitajiki tena, mbali wanasayansi wa kompyuta kutoka MIT (Massachusetts Institute of Technology),” akasema kwenye mtandao wa Twitter.
Alisema hayo huku serikali ya Amerika ikitetea usalama wa ndege za Boeing 737 MAX 8, nayo mataifa zaidi yakipiga marufuku utumizi wa ndege hizo baada ya ajali iliyosababisha vifo vya watu 157 Jumapili.
Jana Uingereza, Australia, Malaysia, Singapore, Australia, Afrika Kusini, Brazil na Mexico zilijiunga na mataifa ambayo yalizuia utumizi wa ndege hizo huku ikiripotiwa marubani Argentina walisusia kuziendesha wakihofia usalama wao.
Lakini Mamlaka ya Kitaifa ya Ndege nchini Amerika (FAA) ilituma taarifa kimataifa kuhakikisha usalama wa ndege hizo.
Ajali ya Jumapili ilikuwa ya pili ya aina hiyo ya ndege katika kipindi kifupi. Oktoba mwaka uliopita, ndege aina hiyo iliyomilikiwa na shirika la Lion Air ilianguka Indonesia na kuua watu 180.
Ilibainika kuwa baada ya ajali ya Indonesia, Boeing iliagizwa na FAA kurekebisha programu za ndege hiyo ambazo zinashukiwa na wataalamu kusababisha ajali.
Imefichuka pia kampuni hiyo imekuwa ikiendeleza mikakati ya kutengeneza upya miongozo ya mafunzo kwa marubani.
Kufikia sasa, kuna jumla ya ndege 387 za aina hiyo zinazomilikiwa na mashirika mbalimbali ulimwenguni.
Huku hayo yakijiri, familia na marafiki wa rubani Yared Getachew walianza kumiminika Mombasa kwa ajili ya swala za mwisho za Kiislamu kwa mwendazake ambaye ni raia mwenye asili ya Kenya na Ethiopia.
Mjombake marehemu, Bw Khalid Shapi alisema swala za mwisho zitafanyika katika msikiti wa Baluchi.
Katika Kaunti ya Kisii, familia katika kijiji cha Mesisita, Kaunti ndogo ya Kisii Kusini, inaomboleza mpendwa wao. Bi Ann Birundu aliyekuwa akisomea uhandisi katika chuo cha Boku, Austraria.