Habari

Himizo serikali na mashirika kuwapelekea msaada wakazi wa vijiji vya Boni wanaokabiliwa na baa la njaa

October 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI wapatao 3,000 wa vijiji vya msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu wanakabiliwa na njaa, hali ambayo imewasukuma wengi wao kujitafutia matunda na mizizi msituni kutumika kama chakula.

Vijiji vinavyokabiliwa na tatizo hilo ni pamoja na Milimani, Basuba, Mangai, Mararani, Pandanguo, Madina na Kiangwe.

Vijiji hivyo hukaliwa na jamii ya walio wachache ya Waboni.

Taifa Leo ilizuru vijiji hivyo juma hili na kubaini kuwa wakazi wengi wanalazimika kuingia msituni kuchuma matunda ya mwitu ili kulisha familia zao kutokana na uhaba wa chakula unaoshuhudiwa eneo hilo.

Wakazi walisema licha ya kujitahidi kulima mashamba yao mwaka huu, hakuna mavuno yoyote walipata kutokana na wadudu pamoja na wanyama pori waliovamia na kuharibu mimea yao.

“Hatuna chakula na maji hivyo tunalazimika kuingia msituni kuchuma matunda ili kulisha wake na watoto wetu na tusipofanya hivyo tutakufa njaa kwa sababu hakuna mavuno yoyote tulipata eneo hili,” akasema mkazi wa Milimani Bw Musa Abatika.

Naye Bi Fatma Barissa alisema watoto wao huenda wakaugua utapiamlo kutokana na kukosekana kwa lishe bora.

Ameiomba serikali na wahisani kujitolea na kupeleka misaada ya chakula vijijini mwao.

Kwa upande wake, Msemaji wa Jamii ya Waboni, Ali Sharuti ameielekezea serikali lawama kwa kukosa kutimiza ahadi ya kuwasambazia wakazi wanaoishi msitu wa Boni chakula katika kipindi chote ambacho operesheni inayoendelea – Operesheni Linda Boni – inayolenga kuangamiza na kusambaratisha wapiganaji wa al-Shabaab.

Operesheni hiyo ilizinduliwa Septemba 2015.

“Serikali ilituahidi kwamba tungepewa misaada ya chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu kipindi chote cha operesheni. Jamii yetu kwa sasa haisaidiwi. Msitu pia wameukataza sisi kuingia kujitafutia matunda. Tungeomba wazingatie hilo na watusaidie,” akasema Bw Sharuti.