HabariSiasa

Jubilee yameza Wiper na CCM

June 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

LEONARD ONYANGO na VALENTINE OBARA

UUNDAJI wa Serikali ya mseto chini ya Rais Uhuru Kenyatta sasa unakaribia kukamilika baada ya chama anachoongoza cha Jubilee kumeza rasmi vyama vya Wiper na Chama cha Mashinani (CCM).

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa CCM Isaac Ruto, walitia saini mkataba wa maelewano na Jubilee jana katika makao makuu ya chama hicho tawala mtaani Pangani, Nairobi.

Bw Musyoka alifichua kuwa janga la virusi vya corona lilitatiza mpango wa Wiper kutaka kujiondoa kutoka katika muungano wa NASA unaojumuisha ODM, Amani National Alliance (ANC), CCM na Ford Kenya.

“Kwa sasa chama cha Wiper hakiwezi kufanya muungano na Jubilee kwani bado tuko ndani ya NASA,” akasema Bw Musyoka aliyekuwa akizungumza baada ya hafla ya kutia saini mkataba huo.

“Lakini tunatamani kufanya muungano wa kisiasa na Jubilee; baada ya janga la virusi vya corona tutashauriana na wanachama ili waturuhusu kujiondoa katika muungano wa NASA tuingie kabisa ndani ya Jubilee,” akaongezea.

Kufuatia hatua hiyo, Rais Kenyatta sasa amefanikiwa kutia kibindoni vyama vinne vikuu nchini ambavyo ni ODM inayoongozwa na Raila Odinga, Kanu inayoongozwa na Seneta wa Baringo Gideon Moi, Wiper na CCM.

Mkataba wa Rais na Bw Odinga, almaarufu kama handisheki ndio ulikuwa wa kwanza baada ya uchaguzi wa 2017. Kwa upande mwingine, Kanu ilikubali kuunda muungano na Jubilee hivi majuzi.

Vyama vikuu vilivyosalia nje ni Amani National Congress inayoongozwa na Bw Musalia Mudavadi, na Ford-Kenya inayoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Vyama hivyo viwili vimekuwa vikikumbwa na misukosuko ya uongozi katika siku za hivi majuzi, watetezi wa viongozi hao wawili kutoka Magharibi wakidai mizozo imefadhiliwa na watu wanaotaka kuwalazimisha waingie serikalini.

Hatua iliyochukuliwa jana imetokea wakati ambapo kuna fununu kuhusu mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa katika baraza la mawaziri na usimamizi wa taasisi mbalimbali za serikali.

Duru zilisema kuwa, mawaziri na maafisa wa serikali wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto huenda wakatemwa ili nafasi zao ziende kwa ‘marafiki wapya’ wa Rais Kenyatta.

Hata hivyo, Bw Musyoka alisema yeye binafsi hawezi kutaka kuwa waziri kwa kuwa hilo litamhitaji kujiuzulu kama kiongozi wa Wiper, ilhali anamezea mate urais ifikapo 2022.

Inaaminika hatua hiyo itakuwa mwendelezo wa kiboko ambacho kimekuwa kikielekezwa kwa wandani wa Dkt Ruto katika Seneti na Bunge la Taifa katika wiki zilizopita.

Jana, Jubilee ilikamilisha mpango wake wa kuwatimua wabunge takriban 16 wa kikundi cha Tangatanga kutoka kwa kamati mbalimbali, ambao wakuu wa chama husema wanahujumu ajenda za Rais Kenyatta.

Miongoni mwao ni Cornelly Serem (Aldai), Mbunge Mwakilishi wa Bomet Joyce Korir na mwenzake wa Laikipia Catherine Waruguru.

Katika kikao cha jana, Rais Kenyatta aliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, mwenyekiti Nelson Dzuya na naibu wake David Murathe.

Kadhalika, Mkataba huo unamaanisha kwamba wabunge na maseneta wa chama cha Wiper na CCM sasa watasaidia Rais Kenyatta kusukuma ajenda yake ndani ya Bunge la Kitaifa na Seneti.

Katibu Mkuu wa CCM Zedekiah Bundotich, almaarufu kama Buzeki, alifichua kuwa Rais Kenyatta alianza mazungumzo na gavana wa zamani wa Bomet mara tu baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Kufuatia hatua ya CCM na Kanu kujiunga na mrengo wa Rais Kenyatta, Naibu Rais yumo hatarini kuwa mpweke katika ngome yake ya Rift Valley.