Kaunti yawatengea wavuvi mamilioni
Na WAANDISHI WETU
WAVUVI katika Kaunti ya Mombasa wanatarajia kuvuna pakubwa kwani serikali ya kaunti imetenga Sh250 milioni kuboresha sekta hiyo.
Fedha hizo zitatumika kununua maboti, kujenga vyumba vya kuhifadhi samaki, masoko ya kisasa na kutengeneza maeneo ya wavuvi kuweka vifaa vyao vya kazi na pia sehemu za kuegesha maboti yao.
Kulingana na pendekezo la bajeti ya kaunti ya kipindi cha mwaka wa 2020/2021, serikali ya kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Hassan Joho, itatumia Sh120 milioni kununua maboti hayo, Sh80 milioni kujenga vyumba vya kuhifadhi samaki tani 100, wakati Sh20 milioni zitatumika kuweka soko la kisasa la samaki.
“Kaunti pia itatumia Sh12 milioni kujenga vibanda vya kisasa vya kuuzia samaki na ukumbi wa mikutano katika maeneo ya wavuvi kutua katika maeneo bunge yote,” ilisema ripoti hiyo.
Pia, Sh6 milioni nazo zitatumika katika ujenzi wa mabwawa ya kukuzia samaki.
“Mradi huo unakusudia kuongeza shughuli za uzalishaji wa samaki, kuhakikisha kaunti ina chakula cha kutosha na pia kutoa fursa zaidi za ajira kwa wanawake na vijana,” ikasema.
Angalau maeneo 44 ya wavuvi kutua yatarekebishwa kwa gharama ya Sh10 milioni mara tu bajeti itakapopitishwa. Ununuzi na ukarabati wa maeneo hayo yatafanyika kwa ushirikiano na Halmashauri ya Bandari Nchini (KPA).
Kulingana na ripoti ya mwaka wa 2015 ya shirika la Haki Yetu, kuna maeneo 50 ya wavuvi kutoka Mombasa ambayo yalikuwa yamenyakuliwa.
Wavuvi katika kaunti hiyo walifurahia mpango huo, lakini wakaiomba serikali hiyo iwe ya kusema na kutenda.
“Tunajua kuwa ikiwa mipango yote ambayo imewekwa itatekelezwa, basi tutakuwa na uzalishaji mzuri wa samaki. Tunahitaji msaada wote muhimu ili tasnia yetu istawi,” alisema Khamis Abdallah, mwenyekiti wa wavuvi katika maeneo ya uvuvi katika maeneo ya Old Town.
Kwingineko, Bunge la Kaunti ya Kilifi limepitisha bajeti ya Sh13.3 bilioni ya mwaka wa fedha wa 2020/2021.
Mwenyekiti wa kamati ya bajeti katika bunge hilo Albert Kiraga, alisema bajeti ya mwaka huu imepungua kwa Sh1.4 bilioni ikilinganishwa na ile ya mwaka 2019/2020.
Akiwahutubia wanahabari, alisema wizara ya Afya ndiyo iliyopata mgao mkubwa zaidi wa Sh3.1 bilioni.
Ripoti za Diana Mutheu, Mohamed Ahmed na Alex Amani