Habari

Ni safari tu! Kaunti zatumia mamilioni ziarani kwa miezi mitatu tu

Na COLLINS OMULO December 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAUNTI za Kitui, Kajiado na Kakamega ni miongoni mwa ambazo zimetumia pesa nyingi zaidi kwa safari za ndani na nje ya nchi kwa afisa wa kaunti na madiwani, ripoti mpya inaonyesha.

Kulingana na ripoti ya hivi karibuni kutoka kwa Mdhibiti wa Bajeti, Margaret Nyakang’o, kaunti 36 zimetumia zaidi ya Sh500 milioni kwenye safari katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26. Julai hadi Septemba 2025..

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba nchi zinazopendelewa zaidi kwa safari za nje ni Amerika, Uingereza na Mashariki ya Kati, huku Tanzania ikiongoza barani Afrika.

Kaunti ya Kitui ilitumia zaidi ya Sh106 milioni kwa safari za ndani, ambapo Bunge la Kaunti lilifyonza Sh38.57 milioni na serikali ya Kaunti Sh68.10 milioni.

Kaunti ya Kajiado ilifuata kwa karibu, ikitumia Sh89.9 milioni, Bunge ya kaunti (Sh43.81 milioni) na Serikali ya (Sh46.17 milioni). Safari za nje ziligharimu kaunti hiyo Sh3.49 milioni, zote zikihusishwa na Bunge.

Katika Kajiado, maafisa sita wa Bunge walisafiri Ghana kwa mkutano wa Hansard Association kati ya Agosti 11 na 16, kwa gharama ya Sh1.67 milioni. Wawili walihudhuria warsha ya usimamizi wa fedha Singapore kati ya Julai 13 hadi 21, wakitumia Sh1.25 milioni, huku afisa mmoja akisafiri Urusi kwa warsha ya kisheria kwa gharama ya Sh532,068.

Kaunti ya Kakamega ilipata nafasi ya tatu, ikitumia Sh75 milioni kwa safari za ndani, hasa za madiwani (Sh70.45 milioni). Safari za nje ziligharimu Sh12.18 milioni, sehemu kubwa ikiwa ya madiwani.

Kaunti nane hazikutumia pesa zozote kwa safari za ndani au nje wakati huo: Baringo, Garissa, Nairobi, Narok, Nyandarua, Siaya, Trans Nzoia na Turkana. Ripoti haikuonyesha data za safari kuhusu kaunti za Kilifi, Elgeyo Marakwet na Wajir.

Katika mwaka wa fedha 2018/19, Wizara ya Ugatuzi ilianzisha kanuni inayohitaji madiwani kupata idhini kabla ya safari za nje, kueleza gharama na kuonyesha faida kwa kaunti, baada ya kubaini kuwa ziara hizi ni njia muhimu ya matumizi mabaya ya pesa za umma. Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa sasa safari za ndani ndizo zinazogharimu zaidi.